Boma Hai FM

Ushirikiano wadau wa maendeleo na serikali kukuza sekta ya elimu

20 July 2026, 2:22 pm

Pichani ni diwani wa kata ya Mnadani Emmanuel Mgonja (wa tatu kulia) pamoja na viongozi wa shule ya msingi Mijengweni na kijiji cha Mijongweni (picha na Anasta Urio)

Shirika la FTK limetoa msaada wa samani za darasani kwa Shule ya Msingi Mijongweni ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuunga mkono maendeleo ya elimu.

Na Anasta Urio

Hai- Kilimanjaro

Wananchi na wadau wa maendeleo katika Kata ya Mnadani, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kuunga mkono jitihada za kuinua na kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Pichani ni afisa miradi wa shirika lisilo la kiserikali la FTK Ahmed Rafiki akimkabidhi mwenyekiti wa shule ya msingi Mijongweni samani za viti (picha na Anasta Urio)

Wito huo umetolewa Julai 13, 2026 na Diwani wa Kata ya Mnadani Emanuel Mgonja, wakati wa kupokea msaada wa samani za darasani uliotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la FTK linalofanya kazi chini ya Kampuni ya Sukari ya TPC kwa ajili ya Shule ya Msingi Mijongweni.

Sauti ya diwani wa kata ya Mnadani Emmanuel Mgonja

Msaada huo unajumuisha viti 33 na meza 10 kwa wanafunzi wa darasa la awali ambao hapo awali walikuwa wakilazimika kukaa kwa kusomgamana kutokana na uhaba wa samani za kujifunzia.

Pichani ni samani za viti vilivyokabidhiwa katika shule ya msingi Mijongweni.(picha na Anasta Urio)

Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Miradi wa FTK, Ahmed Rafiki, amesema shirika hilo limeguswa kutoa msaada huo kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya uongozi wa kata hiyo na FTK, huku akiutaka uongozi wa shule kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa ili viweze kuwahudumia wanafunzi kwa muda mrefu.

Sauti ya afisa mradi wa FTK Ahmed Rafiki

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mijongweni Anicent Bruno, amelishukuru shirika hilo kwa kusaidia kutatua changamoto ya upungufu wa samani za darasani, akisema hatua hiyo itachangia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ubora wa elimu shuleni hapo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Miradi ya FTK, Mashati Mwingira, amelipongeza shirika hilo kwa mchango huo na kuomba ushirikiano zaidi katika kuendelea kuimarisha sekta ya elimu katika eneo hilo.

Aidha Mwenyekiti wa Kijiji cha Mijongweni na mwenyekiti wa shule hiyo, Bakari Malola pamoja na baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo, wameahidi kuwahimiza watoto kutunza vifaa hivyo ili viweze kuwanufaisha wanafunzi wa sasa na vizazi vijavyo vitakavyosoma katika shule hiyo.

Sauti ya Mwenyekiti wa shule hiyo pamoja na wananchi