Boma Hai FM
Boma Hai FM
4 September 2026, 12:41 am

Mkuu wa wilaya ya Hai pamoja na wataalamu wa wilaya ya Hai wamekagua ujenzi wa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa ndani ya wilaya na kuridhishwa na ujenzi, akitoa wito kukamilisha miaradi kwa wakati na ubora.
Na Henry Keto, Hai-Kilimanjaro
Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Hassan Bomboko, amewapongeza wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maendeleo wilayani Hai kwa kuzingatia muda, ubora na thamani ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Bomboko ametoa pongezi hizo Septemba Mosi mwaka 2026 wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Hai, ambapo ametembelea miradi mitatu.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Soko la Mula unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni moja, ujenzi wa jengo la Mkurugenzi unaogharimu zaidi ya shilingi milioni 400, pamoja na ujenzi wa jengo jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Hai lenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni nne.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko, amempongeza mkandarasi anayejenga nyumba ya mkurugenzi na jengo jipya la halmashauri PARIC INTERNATIONAL LIMITED kwa kuonesha weledi katika utekelezaji wa miradi hiyo, akisisitiza umuhimu wa wakandarasi kuzingatia ubora na kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi.
Bomboko amesema wakandarasi wanaoonesha juhudi, weledi na kuzingatia ubora pamoja na thamani ya fedha wanapaswa kupewa nafasi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya ya Hai kwa manufaa na maslahi mapana ya wananchi wote.
Aidha, amewataka wakandarasi wote wanaotekeleza miradi wilayani Hai kuhakikisha wanakamilisha miradi kwa wakati, kuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa na kuhakikisha miradi hiyo inaendana na thamani ya fedha zilizotumika.

Akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa jengo la Mkurugenzi na jengo jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Mhandisi wa Wilaya ya Hai, Arnold Matandiko, amesema miradi hiyo inayotekelezwa na kampuni ya PARIC INTERNATIONAL LIMITED inaendelea vizuri, huku ikisimamiwa kwa karibu na Ofisi ya Mhandisi wa Wilaya ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati kwa mujibu wa mikataba.