Boma Hai FM
Boma Hai FM
21 September 2026, 4:20 pm

Mratibu wa maafa wilaya ya Hai Msafiri Msuya, amesema maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua hizo yanahusisha ushirikiano wa idara mbalimbali, ikiwemo afya, kilimo na mifugo, huku wananchi wakitakiwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu na kuepuka maeneo hatarishi.
Na Stanley Christian
Wananchi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuchukua tahadhari za awali kukabiliana na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba hadi Februari 2027, kwa kufanya usafi katika maeneo yao, kuhifadhi chakula na vifaa vya kupikia, pamoja na kutoa chanjo kwa mifugo.
Mratibu wa maafa wilaya ya Hai, Msafiri Msuya ameyasema hayo Septemba 21, 2026, katika kipindi cha Siku Mpya kinachorushwa na Radio Boma Hai FM.
Msuya amesema wananchi wanapaswa kujiandaa mapema kwa kuhifadhi majiko, kuni na mkaa ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua hizo, hususan katika maeneo yanayoweza kukumbwa na mafuriko.
Aidha ameipongeza kamati elekezi ya wilaya ya Hai inayoongozwa na mkuu wa wilaya Hassan Bomboko, pamoja na kamati ya Wataalamu inayoongozwa na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri, kwa kutembelea maeneo hatarishi na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na athari za mvua hizo.
Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Hai ina kongani 15 zinazohusisha majukumu ya idara mbalimbali, ikiwemo Idara ya Afya, ambayo imepewa jukumu la kuimarisha elimu ya usafi wa mazingira na maandalizi ya dawa na tiba za kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, ikiwemo kipindupindu.
Kwa upande wa kilimo Msuya amesema mvua hizo zinaweza kuwa na faida na hasara, hivyo wakulima wanapaswa kupanda mazao yanayoweza kustahimili maji mengi, huku wananchi wanaofuga katika maeneo ya mabonde wakitakiwa kuhamisha mifugo yao kwenda maeneo salama.