Boma Hai FM
Boma Hai FM
8 October 2026, 2:13 pm

Katika wiki ya huduma kwa wateja inayoadhimishwa kila mwaka Octoba 5-7, HRT Saccos wamefanya shughuli mbalimbali za huduma bora kwa wateja ikiwa ni pamoja na kuwatembelea wanachama wao wenye changamoto za afya.
Na Gasper Mushi & Juma Robert
Hai – Kilimanjaro
Meneja wa Chama cha Akiba na Mikopo Hai Rural Teachers SACCOS Upendo Lyatuu amesema huduma kwa wateja haipaswi kuwa jambo la wiki ya huduma kwa wateja pekee, bali inapaswa kuwa sehemu ya utamaduni wa kila siku wa kuwajali na kuwathamini wanachama.
Lyatuu amesema hayo Oktoba 5, 2026 wakati uongozi wa Hai Rural Teachers SACCOS ulipomtembelea na kumpelekea mahitaji mbalimbali mwanachama wao na mwalimu mstaafu Khadija Shabani Swai ambaye anachagamoto ya afya ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja.
Amesema HRT Saccos imekuwa na utamaduni wa kuwatembelea na kuwafariji wanachama wake pamoja na jamii yenye uhitaji, akiwataka wananchi kuiga mfano huo kwa kuwa na utamaduni wa kuwajulia hali wagonjwa na wahitaji mara kwa mara.
Amesema ziara hiyo imelenga kuonyesha upendo kujali na kuthamini wanachama ambao wamekuwa sehemu ya Hai Rural Teachers SACCOS kwa muda mrefu, pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya SACCCOS na wanachama wake.
Kwa upande wake Khadija Shabani Swai ameishukuru Hai Rural Teachers SACCOS kwa kumtembelea na kumjulia hali, akisema kitendo hicho kimempa faraja kubwa na kumfanya ajisikie kuthaminiwa.
Hai Rural Teachers SACCOS inaadhimisha wiki ya huduma kwa wateja ikiwa na kauli mbiu “The Extra Mile ,Nyuma ya kila huduma bora kuna timu bora na inayojali.”