Boma Hai FM
Boma Hai FM
17 August 2026, 10:09 am

Hai Teachers SACCOS yazidi kuimarika kifedha, huku mtaji ukikua kwa asilimia 14 na utoaji wa mikopo ukiongezeka kwa zaidi ya asilimia 20 ,Wanachama wapatiwa elimu ya fedha kuhusu nidhamu ya matumizi, umuhimu wa akiba, uwekezaji na matumizi sahihi ya mikopo ili kujenga uhuru na ustawi wa kifedha.
Na Elizabeth Mafie
Hai-Kilimanjaro
Chama cha Akiba na Mikopo cha Hai Teachers SACCOS kilichopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, kimesema kimeendelea kuimarika katika ukuaji wa mtaji, akiba na utoaji wa mikopo, huku watumishi wa serikali wakihimizwa kujiunga na vyama vya ushirika ili kunufaika na huduma za kifedha kwa gharama nafuu.
Mwenyekiti wa Hai Teachers SACCOS, Baraka Elisante Owenya, ameyasema hayo Agosti 15, 2026 katika ukumbi wa KKKT Hai Mjini, wakati wa mkutano wa kukusanya dondoo uliowakutanisha takribani wanachama 800 kutoka Wilaya ya Hai.

Amesema mkutano huo umelenga kutoa elimu na mafunzo kwa wanachama pamoja na kuwapa fursa ya kutoa maoni na mapendekezo yatakayotumika katika maandalizi ya Mkutano Mkuu wa mwaka 2026.
Owenya amesema SACCOS hiyo inayohudumia watumishi wa serikali kuu, serikali za mitaa pamoja na watumishi wa sekta binafsi, imeendelea kupata mafanikio katika ongezeko la wanachama, akiba, amana na mtaji.

Amesema hisa, akiba na amana zimeongezeka kwa asilimia 12 ikilinganishwa na mwaka uliopita, huku mtaji ukiongezeka kwa asilimia 14 na utoaji wa mikopo ukiongezeka kwa zaidi ya asilimia 20.
Amesema Hai Teachers SACCOS inatoa huduma katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kilimanjaro ikiwemo Hai, Siha na Rombo, huku ikiwakaribisha watumishi kutoka maeneo mbalimbali kujiunga na chama hicho bila kujali wanafanya kazi wilaya gani.
Owenya amesema mwanachama wa SACCOS hiyo anaweza kupata mkopo kwa riba ya asilimia 11 kwa mwaka, akisisitiza kuwa vyama vya ushirika si taasisi za unyonyaji, bali ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wanachama kiuchumi.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Dkt. Beatrice Kimaro, ambaye alikuwa mwezeshaji wa semina hiyo, amesema elimu ya fedha ni muhimu kwa watumishi na wastaafu kwa kuwa inawasaidia kupanga bajeti, kuweka vipaumbele, kujiwekea akiba na kutafuta vyanzo zaidi ya kimoja vya mapato.

Dkt. Kimaro amesema utegemezi wa mshahara pekee unaweza kuleta changamoto katika kukidhi mahitaji ya kila siku, huku matumizi yasiyo na mipango pamoja na madeni yakiweza kusababisha baadhi ya watumishi kupoteza uhuru wao wa kifedha na kukabiliwa na msongo wa mawazo.
Amesema elimu ya fedha inapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa inamwezesha mtu kufanya uwekezaji, kuweka akiba kwa ajili ya dharura na kupanga maisha yake wakati akiwa kazini, anapostaafu na hata baada ya kustaafu.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama, wa Hai Teachers SACCOS Mwalimu Onesmo Joseph Nasari, amesema semina hiyo imewasaidia kuelewa namna sahihi ya kutumia fedha na mikopo na kwamba elimu hiyo imewafundisha umuhimu wa kukopa kwa ajili ya mahitaji yenye tija badala ya kutumia mikopo katika matumizi yasiyo ya lazima.
Hata hivyo Mwalimu Asha Hussein Doti, ambae pia ni mwanachama wa Hai Teachers SACCOS amesema semina hiyo imemsaidia kujifunza namna ya kupanga bajeti, kuweka akiba na kutumia mikopo kwa matumizi sahihi.
Ameeeza kuwa elimu itamsaidia kuepuka matumizi yasiyo ya lazima na kumwezesha kutimiza malengo aliyojiwekea na kwamba amedhamiria kuanza kufanya mabadiliko katika matumizi yake ya fedha baada ya kupata elimu hiyo.
