Boma Hai FM

Kwasadala wahimizwa kuzingatia lishe bora, kushiriki mapokezi ya mwenge 2026

29 June 2026, 7:54 am

Pichani ni afisa lishe Irene Shoo akitoa elimu kwa wananchi wa kijiji cha Kwasadala.(picha na Mwandishi wetu)

Wananchi wamekumbushwa umuhimu wa kula mlo kamili, kudumisha usafi wa mazingira na kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru utakaopitia wilayani Hai, huku miradi ya maendeleo ikitarajiwa kuzinduliwa.

Na Elizabeth Mafie

Hai- Kilimanjaro

Wananchi wa kijiji cha Kwasadala kata ya Masama kusini wilayani Hai mkoani Kilimanjaro  wameaswa kuzingatia ulaji wa makundi mbalimbali ya vyakula ili kuimarisha zaidi afya zao jambo litakalowafanya wazidi kujikita zaidi katika suala la maendeleo.

Akizungumza na wananchi hao katika maadhimisho ya lishe ambayo hufanyika kila baada ya miezi mitatu Afisa Lishe kutoka kata ya Masama Kusini Irene Shoo amesema kuwa ulaji wa makundi mbalimbali ya vyakula unaongeza uimara wa afya za wananchi pamoja na kuusaidia mwili kutokupata magonjwa mbalimbali.

Pichani ni aina mbalimbali za nafaka ambazo zimetumika kama njia ya kufikisha elimu ya lishe kwa jamii(picha na mwandishi wetu)

“Tukizingatia lishe bora na ulaji wa makundi yale sita ya vyakula ikiwemo vyakula vyenye Protini, wanga, mbogamboga, matunda na maji itasaidia miili yetu kuwa imara na kama hatusumbuliwi na magonjwa basi tunaweza kujikita zaidi katika uzalishaji na shughuli nyingine za kimaendeleo”. Amesema Irene Shoo

Kwa upande wake Afisa mtendaji wa kijiji cha  Kwasadala Edwine Lamtey amesema kuwa maadhimisho hayo hufanyika kila baada ya miezi mitatu ikiwa ni njia ya kuikumbusha jamii juu ya kuzingatia mlo bora.

“Mambo ya lishe bora ni msingi wetu bora wa maendeleo maana hakuna maendeleo bila lishe bora, na hapa tunazungumzia ulaji wa makundi yale ya vyakula, usafi wa mazingira pamoja na uwepo wa vyoo bora katika makazi yetu”. Amesema Lamtey

Katika hatua nyingine Lamtey ametumia  nafasi hiyo kuwahamasisha wananchi wa kijiji cha Kwasadala   kushiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru ambao unatarajiwa  kuwasili  wilaya ya Hai  Julai 3,2026

Sauti ya afisa mtendaji kijiji cha Kwasadala Edwine Lamtey

“Nawaomba wote pia tushiriki kuupokea mwenge wa uhuru wilayani kwetu na zaidi katika kijiji cha kwasadala tutakuwa na miradi miwili ambayo ni mradi wa maji pamoja na kiwanda binafsi; kwa mantiki hiyo tujitokeze kwa wingi katika maeneo ya barabarani na hata maeneo ya miradi”Amesema Lamtey