Boma Hai FM

Wanawake kutumia siku ya wanawake duniani kukuza uchumi

3 March 2026, 3:39 pm

Pichani ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya siku ya wanawake duniani wilaya ya Hai Andogwitse Ndelwa(picha na Salma Mgosso)

Zikiwa zimesalia siku chache kuelekea siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka machi 8 kote duniani,wilaya ya Hai imejipanga kuadhimisha siku hiyo katika viwanja vya shule ya sekondari Mailisita Jumatatu machi 9 2026.

Na Anasta Urio

Hai-Kilimanjaro

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi  8 wanawake wilayani Hai  mkoani Kilimanjaro wameaswa kuitumia siku hiyo kama fursa ya kuboresha biashara zao, kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali, na kukuza uchumi wao pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Wanawake Andogwitse Ndelwa alipokuwa akizungumza na Radio Boma  Fm Marchi 2, 2026 na kwamba katika maadhimisho hayo yatafanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Mailisita   Marchi 9 , 2026 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mh Nurdini Babu.

Aidha amewataka wanawake wote kujitokeza kwa wingi kusherehekea na kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa kushiriki katika zoezi la usafi ndani na nje ya Hospitali ya Wilaya pamoja na kuchangia damu kwa ajili ya wagonjwa ambapo zoezi  hilo litafanyika Marchi  6, 2026 kuanzia saa mbili asubuhi katika Hospitali ya Wilaya ya Hai, ikiwa ni sehemu ya matendo ya huruma kwa wenye uhitaji.

Sauti ya mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya siku ya wanawake duniani wilaya ya Hai Andogwitse Ndelwa.

Kwa upande wake afisa manunuzi wilaya  ya Hai  Nance Nyali amesema kuwa maadhimisho hayo yanawahusu wanawake wote wa Mkoa wa Kilimanjaro na kwamba kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kunawasaidia wanawake kujitambua na kuwa na ujasiri katika kufanya maamuzi yatakayochochea maendeleo yao binafsi na ya jamii kwa ujumla.

Naye Afisa wa Afya wa Wilaya ya Hai Upendo Sheyo amewahimiza wanawake wa wilaya ya Hai  na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kimkoa yatafanyika wilayani Hai. Maadhimisho hayo yataongozwa na kauli mbiu isemayo “Haki na usawa kwa wanawake na wasichana msingi jumuishi kufikia dira 2050”