Boma Hai FM

NSSF Hai watoa msaada kuelekea siku ya wanawake duniani

8 March 2024, 8:45 am

Afisa msimamizi wa NSSF wilaya ya Hai na Siha Pamela Mallya pamoja na watumishi wengine wakikabidhi vitu mbalimbali katika ofisi ya maendeleo ya jamii wilaya ya Hai(picha na Stanley Chstian)

Katika kuelekea siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Machi 8 kila mwaka NSSF wilaya ya Hai wametoa msaada kwa wenye uhitaji.

Na Stanley Christian

Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wametembelea ofisi za maendeleo ya jamii katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro lengo likiwa ni kutoa misaada ya taulo za kike, madaftari pamoja na kalamu kwa watoto wa kike.

Sauti ya Pamela Malya afisa msimamizi NSSF wilaya za Hai na Siha.

Afisa msimamizi wa NSSF wilaya ya Hai na Siha Pamela  Mallya amesema wao kama shirika la taifa la hifadhi ya jamii wanatambua mchango wa maadhimisho hayo hivyo hawana budi kushirikiana na jamii ili kuhakikisha kilele cha siku ya wanawake wanasherekea vyema.

Amesema kuwa baadhi ya vitu walivyotoa katika ofisi hizo za maendeleo ya jamii ni taulo za kike 120, madaftari 100 pamoja na kalamu 200 lengo likiwa  ni kuwasaidia watoto wa kike kufanya vyema katika masomo yao na kuondokana na changamoto  wanazokutana nazo kwa maeneo ya vijijini.

Aidha amewataka wanawake katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo kwa kuchagua viongozi watakaokuwa msaada kwa jamii  na kuleta maendeleo.

Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa wilaya ya Hai yatafanyika katika kata ya Narumu ambapo wanawake mbalimbali katika wilaya ya Hai watakutana kwa ajili ya hafla hyo siku Ijumaa Machi 8, 2024.