Boma Hai FM

HRT watoa msaada kwa wanafunzi wenye uhitaji

21 December 2023, 9:52 pm

Mwenyekiti wa chama cha ushirika wa akiba na mikopo Hai Rural Teachers SACCOS (HRT) Mwalimu Alex Warioba akikabidhi sare za shule kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu (Picha na Elizabeth Mafie)

Chama cha ushirika wa akiba na mikopo Hai Rural Teachers SACCOS (HRT) wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kimetoa msaada wa sare za shule kwa wanafunzi wenye uhitaji kutoka shule 16 za wilaya ya Siha.

Na Elizabeth Mafie

Chama cha Ushirika wa  Akiba na Mikopo (Hai Rural Teachers SACCOS (HRT)  kilichopo  wilayani Hai mkoa wa Kilimanjaro  kimekabidhi msaada wa sare za shule  kwa wanafunzi 55  wanaoishi katika mazingira magumu kutoka katika shule 16 za  wilaya ya Siha huku wazazi na walezi wilayani humo wakitakiwa kuwasimamia watoto wao shuleni ili waweze kusoma kwa bidii na kuweza kutimiza ndoto zao.

Msaada huo  wenye thamani ya shilingi milioni mbili umekabidhiwa katika eneo la shule ya msingi Sanya Juu na Mwenyekiti wa chama hicho  Mwalimu Alex Warioba ambapo amesema  matendo hayo ya huruma waliyofanya ni sehemu ya  misingi  ya vyama vya ushirika na kwamba wana misingi  saba na msingi  mmojawapo  ni kuijali jamii na kwamba watoto hao wapelekwe shule kwani shule zimejengwa, madawati ya kutosha na wao wameamua kutoa sare hizo.

Amesema kuwa wamegusa shule 16  ambapo watoto 55 wanaotoka shule tofauti tofauti za wilaya ya siha, ambao  wanasoma darasa la kwanza hadi la sita, wameshonewa  sare za shule.

Sauti ya mwenyekiti wa Hai Rural Teachers SACCOS (HRT) Mwalimu Alex Warioba.

Kwa upande wake meneja wa chama hicho Upendo Lyatuu amesema kuwa chama hicho kina utaratibu wa kila mwaka  kutenga kile wanachokipata kama faida kwenye chama  kwa ajili ya kuijali jamii wana utaratibu wa kupokeza  katika  wilaya mbili kwa kuwa  wanachama wao wanatoka katika wilaya ya Hai   pamoja na Siha hivyo  mwaka jana walitoa wilaya ya Hai na mwaka huu wametoa wilaya ya Siha na waliona ni vyema kuwagusa wale wanafunzi ambao wanatoka katika mazingira magumu kwa kuwashonea sare za shule ili nao waweze kujisikia vizuri kama wanafunzi wengine.

Upendo amewaomba wanafunzi hao kusoma kwa bidiii kwani wao kama chama watafurahi kuwaona wanafunzi hao wameshasoma na kufanikiwa kuwa kwenye ajira na wamejiunga na kuwa wanachama wa chama hicho.

Amesema Chama hicho kina jumla ya wanachama wapatao 2560 kwa sasa ambao wanatoka katika wilaya za Siha na Hai.

Sauti ya meneja wa Hai Rural Teachers SACCOS (HRT) Upendo Lyatuu.

Kwa upande wao wazazi wa  watoto hao na mwalimu Frank Mariki pamoja  wanafunzi  waliopatiwa sare  hizo walishukuru chama hicho cha akiba na mikopo kwa kuwajali wanafunzi wao ambapo wamesema  wanafunzi hao wanaishi katika mazingira  magumu kwani hawana  namna  ya kujitetea kifedha.

Sauti ya Mzazi wa mwanafunzi aliyepatiwa sare za shule Mursale Ndosi akishukuru chama hicho kwa kuwapatia msaada na kuhaidi kuwasimamia watoto hao ili waweze kusoma kwa bidii.