Boma Hai FM

Wanafunzi wasiokuwa na sare kuendelea na masomo

5 January 2024, 11:23 pm

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake (picha na Janeth Joseph)

Zikiwa zimebaki siku chache shule za msingi na sekondari kufunguliwa hapa nchini mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu atoa wito kwa wakuu wa shule.

Na Elizabeth Mafie

Wito umetolewa kwa wakuu wa shule za msingi na sekondari katika mkoa wa Kilimanjaro kutokuweka vikwazo kwa wanafunzi wanaotarajia kurejea mashuleni siku za hivi karibuni na kwamba ni marufuku kumzuia kuendelea na masomo mwanafunzi ambae hana sare.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdini Babu hii  leo, wakati akizungumza na waandishi wa habari  ofisini kwake ambapo amesema suala la mwanafunzi kutokua na  viatu au sare za shule lisimfanye mwalimu kumrudisha mwanafunzi nyumbani kwa kuwa  mengine yanazungumzika mwanafunzi akiwa darasani.

Hata hivyo,  amesema ni marufuku wakuu wa shule kuendesha michango isiyo kuwa  ya lazima mashuleni na kwamba kama kuna michango upo utaratibu wa kufuatwa.

Sauti ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu.

Pamoja na mambo mengine, ametoa rai kwa wazazi na walezi wote katika mkoa wa Kilimanjaro, kuhakikisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wote wanaripoti shuleni bila kisingizio chochote kwa kuwa serikali imefuta ada mashuleni.

Sauti ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu.

Babu amesema kuwa jumla ya wanafunzi 36, 570 wakiwemo wavulana 18,013 na wasichana 18,557 ambao  walifaulu  mitihani yao ya darasa la saba wote watapata nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza katika shule mbalimbali walizochaguliwa .

Hata hivyo, Babu amewakumbusha wazazi na walezi kuchangia chakula mashuleni ili watoto waweze kupata chakula wakiwa shuleni na kwamba   ni jukumu la kila mzazi kutekeleza wajibu huo.