Boma Hai FM
Boma Hai FM
20 June 2026, 10:07 am

Serikali imewahakikishia wananchi wa Narumu na Jimbo la Hai kwa ujumla kuwa juhudi zinaendelea kuhakikisha mradi wa ujenzi wa Chuo cha Afya Narumu na Kituo cha Afya unapata fedha za kutosha ili kukamilika kwa wakati.
Na James Gasindi
Dodoma
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya ili kuharakisha upatikanaji wa fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya na Chuo cha Afya Narumu kilichopo katika Jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro.
Kauli hiyo imetolewa Juni 17,2026 bungeni na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar Sei, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miradi hiyo.
Saashisha ameeleza kuwa wananchi wa Narumu walihamasika kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo baada ya Serikali kutoa ahadi ya kujenga kituo na chuo hicho, ambapo walichangia nguvu kazi, vifaa vya ujenzi na kuanzisha msingi wa majengo yanayotarajiwa kutumika.
Akijibu hoja hiyo, Dkt. Sei alisema Serikali inatambua umuhimu wa vyuo vya afya katika kuzalisha wataalamu wa afya wanaohitajika nchini na kwamba mawasiliano kati ya TAMISEMI na Wizara ya Afya yanaendelea ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo.
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa Chuo cha Afya Narumu kutasaidia kuongeza idadi ya wataalamu wa afya na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
