Boma Hai FM

Mkenda Super Cup 2024 yazinduliwa rasmi, wachezaji wapewa vifaa vya michezo

31 March 2024, 10:35 am

Mkuu wa wilaya ya Rombo Raymond Mangwala pamoja na Mbunge wa Rombo Profesa Adolf Mkenda wakiwa katika uzinduzi wa mashindano ya Mkenda Super Cup 2024 katika viwanja vya sabasaba Mkuu Rombo(picha na Elizabeth Mafie)
Mkuu wa wilaya ya Rombo Raymond Mangwala ambae ndie mgeni rasmi katika mashindano hayo,akiwa na mbunge wa Rombo pamoja na viongozi wengine wakisalimiana na wachezaji wa timu ya Kelamfua Mokala (picha na Elizabeth Mafie)
Mgeni rasmi Raymond Mangwala ambae ndie mkuu wa wilaya ya Rombo akikabidhi vifaa vya michezo kwa wachezaji wa mashindano ya Mkenda Super Cup 2024 (picha na Elizabeth Mafie)

Mashindano ya Mkenda Super Cup ambayo yalianza rasmi mwaka 2022 katika Jimbo la Rombo yakidhaminiwa na Mbunge wa Jimbo hilo Profesa Adolf Mkenda yazinduliwa rasmi,timu za mpira wa miguu zipatazo 126 kuchuana vikali.

Na Elizabeth Mafie

Mashindano ya Mkenda Super Cup 2024 yamezinduliwa rasmi katika viwanja vya sabasaba Mkuu Rombo na Mkuu wa wilaya hiyo Raymond Mangwala ambapo timu  za mpira wa miguu zaidi ya mia moja zinatarajiwa kuchuana.

Akizungumza katika uzinduzi huo mgeni rasmi Raymond Mangwala ambae ndie mkuu wa wilaya ya Rombo amesema kuwa anampongeza mbunge wa jimbo hilo Profesa Adolf Mkenda kwani kwa sasa jimbo la Rombo linaelezea utekelezaji wa ilani inayotekelezwa katika nchi hii  na kwamba yeye kama mwenyekiti wa usalama anaona wilaya inakuwa salama vijana wanapokuwa wameitwa pamoja na wanafanya michezo kwani hawafikirii mambo mengine bali wanafikiria michezo.

“Ukija Rombo unayaona matokeo ya utekelezaji wa ilani inayotekelezwa katika nchi hii kwa hiyo tunavyozungumzia Rombo,tunazungumzia liwilaya likubwa,liwilaya lenye mafanikio,lakini hakuna mafanikio yasiyotengenezwa,mkiona vyaelea mjue vimeundwa na mmoja ya mtu aliyeviunda vitu vya wilaya yetu ni Profesa Adolf Mkenda, hongera sana nije kwenye bodi ya ligi niwapongezeni sana bodi ya ligi kazi nzuri na hii  mnatusaidia  hata sisi kama serikali ,mimi kama mwenyekiti wa usalama ninaona wilaya inakuwa salama vijana wanapokuwa wameitwa pamoja na wanafanya michezo  hawafikirii mambo mengine wanafikiria michezo, ni wilaya salama”Amesema Raymond Mangwala.

Sauti ya Raymond Mangwala Mkuu wa wilaya ya Rombo na mgeni rasmi katika uzinduzi wa mashindano hayo.

Awali akielezea nia na madhumuni ya Mkenda Super Cup mratibu wa mashindano hayo  Temy  Isidory  amesema kuwa mashindano hayo yalianza rasmi mwaka 2022 na kwamba yalianza na zaidi  ya timu  hamsini  lakini kwa sasa wana timu zaidi ya mia moja, hivyo mafanikio ni makubwa na mashindano hayo yameleta tija na fursa kwa vijana kwani michezo inawaepusha na vitendo visivyofaa katika jamii  pamoja na kuwakutanisha vijana ili  wapate kujua kazi mbali mbali zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais  Dr Samia Suluhu Hassani.

Nae mbunge wa  Rombo Profesa Adolf Mkenda ambae pia ndie waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia hapa nchini  na ndie mdhamini wa Mkenda Super Cup amesema kuwa mashindano hayo yatatumika kuwahamasisha vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu uchaguzi wa serikali za mitaa pia yatatumika kueleza kazi ambazo serikali imefanya pamoja na kuwakumbusha miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa Rombo ili watakapofanya uchaguzi wafanye uchaguzi sahihi.

Sauti ya Profesa Adolf Mkenda mbunge wa Rombo na waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia hapa nchini.

Kwa upande wao vijana wanaoshiriki katika mashindano hayo wamemshukuru mbunge wa jimbo hilo Profesa Adolf Mkenda na kwamba mashindano hayo yamekuwa tija na fursa kwao na watayatumia ipasavyo kwani kwa sasa michezo ni ajira huku wakiwasihi vijana wengine kujiunga katika timu za mpira wa miguu ili waweze kunufaika na mashindano hayo.

Katika uzinduzi huo zilichuana  vikali timu ya Kelemfua Mokala na Vunjo Fc kutoka Jimbo la Vunjo ambapo timu ya Kelemfua Mokala kutoka Rombo  ilimchapa bao 4-0 timu hiyo ya Vunjo FC.