Boma Hai FM

Diwani awatuliza wananchi wenye hasira kali

10 December 2023, 6:20 pm

Diwani wa kata ya Masama Kusini Cedrick Pangani akizungumza na wananchi wa kijiji cha mkombozi picha na Bahati Chume.

Wananchi wa kijiji cha mkombozi wataka kubomoa nyumba ya mwananchi mmoja anayedaiwa kuvamia eneo la kijiji.

Na Elizabeth Mafie

Diwani wa kata ya Masama Kusini Cedrick Pangani amewataka wananchi wa kijiji cha Mkombozi Wilayani Hai mkoani Kilimanjaro  kusitisha zoezi la kwenda kubomoa nyumba ya mwananchi mmoja Gabriel Kitika  anayedaiwa kuvamia eneo la Kijiji hicho na kufanya shughuli za kilimo pamoja na  ujenzi. 

Kauli hiyo imekuja baada ya kuwepo zuio kutoka ofisi ya baraza la ardhi la kata kwamba shughuli yoyote zisifanyike hadi hapo itakapo bainika nani mmiliki halali wa eneo hilo ambapo mwananchi huyo alipuuza.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho waliokusanyika  katika eneo  lenye mgogoro huo ,amewataka wananchi hao kuwa wavumilivu na kusitisha zoezi hilo na kufuata taratibu za kisheria na kwamba alipata taarifa uwepo wa wananchi wa Kijiji hicho waliojikusanya kwenda kubomoa nyumba ya mwananchi huyo aliyevamia eneo la Kijiji hicho lenye ukumbwa wa ekari 10 na kuanza ujenzi kitu ambacho ni kinyume na maagizo yaliyotolewa.

Amesema kuwa  mwananchi huyo baada ya uvamizi wa eneo hilo alifikishwa baraza la  ardhi la kata iliyopo kwasadala na kuagizwa  kuacha kufanya shughuli yoyote mpaka hapo itakapobainika nani mmiliki halali wa eneo hilo.

Hata hivyo  mwananchi huyo  hakutaka kufuata maagizo ya baraza  na kuendelea na ujenzi ambapo wananchi walichukizwa na jambo hilo na kuamua wajikusanye kwa lengo la kubomoa nyumba hiyo ambapo Diwani huyo aliwasihi kuacha na kufuata utaratibu.

Sauti ya diwani kata ya Masama Kusini akizungumza kuhusiana na mgogoro huo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji hicho  Fikiri Rezer amesema kuwa  mwaka huu walifika ofisi ya aridhi ya kata na mlalamikiwa  kuamriwa kutoa vielelezo lakini hakutoa na uamuzi uliotolewa ni kutokufanya shughuli yoyote katika eneo hilo mpaka hapo ufumbuzi utakapopatikana,  hata hivyo baada ya mkutano huo  mwananchi huyo amekubali kupeleka vielelezo alivyonavyo vinavyothibitisha umiliki wa eneo hilo katika baraza la ardhi la kata.

Nae mwenyekiti wa baraza la ardhi na nyumba kata hiyo Ally Mmbaga amesema kuwa iwapo eneo lina mgogoro hairuhusiwi  mtu yoyote kufanya shughuli katika eneo hilo na atakaefanya hivyo  atakuwa anatenda  kosa la jinai na  ameutaka uongozi wa Kijiji hicho  pamoja na mwananchi huyo kupeleka vielelezo walivyonavyo ili kuweza kufahamu nani mmiliki halali.

Sauti ya mwenyekiti wa baraza la ardhi na nyumba kata ya Masama Kusini akitoa ufafanuzi wa kisheria.