Wananchi Hai watakiwa kuandaa mazingira ya kudhibiti ukatili
12 December 2023, 9:12 pm
Wananchi Hai wametakiwa kuwajibika kuzuia ukatili wa kijinsia katika jamii.
Na Anasta Urio
Wananchi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuandaa mazingira ya kudhibiti vitendo vya ukatili katika jamii bila kujali siasa, dini pamoja na ukabila ili kuhakikisha kila mtu anawajibika kupinga na kuzuia ukatili wa kijinsia.
Hayo yamesemwa na mgeni rasmi Nsajigwa Ndagile kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Hai Amir Mkalipa katika mkutano wa maadhimisho ya kilele cha kampeni ya siku 16 za kuzuia ukatili wa kijinsia iliyokuwa na kaulimbiu ya “Wekeza kupinga ukatili wa kijinsia” iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya Hai.
Aidha Ndagile ametoa pongezi kwa wadau mbalimbali walioshiriki katika kuhamasisha na kukamilisha kampeni hiyo tangu ilipoanza hadi kufikia siku ya kilele na kwamba wanatakiwa kuendelea kutoa elimu zaidi ili jamii izidi kuelimika.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bomani, Nyangi Ikwabe amesema kuwa ukatili wa kijinsia unaweza kufanywa na mtu yeyote na kuleta madhara katika jamii na kuwataka wazazi kutimiza wajibu wao kwa watoto ili kuwalinda dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Naye mwenyekiti wa jukwaaa la mwanamke wilaya ya Hai Etropia Assenga amesema kuwa kuna aina nyingi za ukatili ikiwemo ukatili wa kingono, ukatili wa kiuchumi, ukatili wa kimwili na ukatili wa kisaikolojia ambao umekuwa ukiwaathiri zaidi wanaume.