Boma Hai FM

Wazazi chanzo cha ukatili kwa watoto

2 January 2024, 7:06 pm

Happiness Maruchu kutoka TGNP akizungumza na wanaharakati wanaopambana na vitendo vya ukatili wilayani Same mkoani Kilimanjaro (Picha na Dickson Mzava)

Baadhi ya wazazi na walezi wametajwa kuwa chanzo cha ukatili kutokana na kutokutoa ushirikiano pindi watoto wao wanapofanyiwa ukatili.

Na Elizabeth Mafie

Imeelezwa kuwa kudidimia kwa ndoto za watoto wengi hasa wa kike wilayani Same mkoani Kilimanjaro kunatokana na baadhi ya wazazi na walezi kuwa chanzo cha ukatili kwa watoto wao.

Wakizungumza kwenye kikao kazi kilichoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP  unaojihusisha na kupinga ukatili, wanaharakati wanaopambana na vitendo vya ukatili Stella Mkwizu na Happiness Elia wamesema wapo baadhi ya watoto ambao wamepoteza haki zao za muhimu hasa elimu kwa kufanyiwa ukatili wa kijinsia na wazazi wao.

Sauti ya mwanaharakati wa kupinga ukatili Stella Mkwizu

Wamesema baadhi ya wazazi huficha ukatili wa kijinsia unaofanywa na baadhi ya watu wasio wema hasa ubakaji, ulawiti, ukeketaji na ndoa za utotoni kwa kile kilichodaiwa wazazi hupokea hongo kutoka kwa mhalifu na kuficha ushahidi wa ukatili kwa mtoto wake.

Happiness Maruchu kutoka TGNP amesema miongoni mwa vitendo vya ukatili ambavyo bado vimekithiri wilayani Same ni pamoja na ukeketaji kwa mtoto wa kike, ulawiti na ndoa za utotoni huku  akiihimiza halmashauri ya wilaya ya Same kutenga bajeti kwa ajili ya vifaa mbalimbali vya kujisitiri shuleni kwa mtoto wa kike pindi anapokuwa kwenye hedhi.

Maruchu amesema uwepo wa chumba salama kwenye shule na taulo za akiba shuleni pamoja na vyoo bora vitamsaidia mtoto wa kike katika kukabiliana na changamoto mbalimbali pindi awapo kwenye hedhi.

Kwa upande wake wakili wa halmashauri ya hiyo Upendo Kivuyo  amesema katika kukabiliana na changamoto zote hizo na kuhakikisha haki inapatikana kwa wote wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia hasa mabinti lazima patungwe sheria ndogondogo.