Boma Hai FM

Dkt Biteko aongoza mamia mbio za Rombo marathon na ndafu festival

24 December 2023, 7:04 pm

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa nishati Dkt Dotto Biteko,Mbunge wa Jimbo hilo Profesa Adolf Mkenda na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu wakiwa na baadhi ya washiriki wa mbio za Rombo marathon na ndafu festival (picha na Elizabeth Mafie)

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa nishati Dkt Dotto Biteko amesisistiza ushiriki wa matukio ya kijamii ikiwemo shughuli za kijamii,michezo na matamasha mbali mbali ikiwa ni njia moja wapo ya kuwakutanisha wananchi na taasisi lakini pia kuwajengea mahusiano mazuri baina yao hali itakayo changia  kukua kwa maendeleo.

Na Elizabeth Mafie

Naibu waziri Mkuu na Waziri wa nishati mheshimiwa  Dkt Dotto Biteko ameshiriki na mamia ya wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na wilaya ya Rombo pamoja na wakazi wa mikoa jirani katika mashindao ya mbio fupi za Rombo marathon na ndafu festival iliyofanyika katika  eneo la hifadhi ya msitu wa Rongai huku akiwataka watanzania kuwa na utamaduni wa kutembelea katika maeneo yao ya asili pamoja na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Akizungumza katika mashindano hayo ya Rombo Marathoni pamoja na ndafu festival amesema kuwa wageni walioshiriki katika mbio hizo ni fursa ya kujifunza utamaduni wa watu wa rombo kwa kurudi nyumbani kipindi cha mwisho wa mwaka na kuungana na familia zao, kwani watu wanaorudi nyumbani wanafanya maboresho pamoja na maendeleo mbalimbali katika jamii kwani lengo la mashindano hayo ni kujenga vyoo katika shule ambazo vyoo vyake ni chakavu  pamoja na kuipandisha hadhi  hospitali ya Huruma iliyopo katika wilaya hiyo na kwamba jambo hilo kwa watu wasiorudi nyumbani ni ngumu kuliona.

Sauti ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa nishati Dkt Dotto Biteko.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia na   mwanzilishi wa mashindano hayo Profesa  Adolf Mkenda  amewashukuru wote waliowezesha kufanyika kwa mashindano hayo na wote walioshiriki katika mbio hizo na kwamba upo mkakati katika kuendeleza mashindano hayo kwani kila mwaka disemba 23 kutakuwa na mashindano ya Rombo marathon na Ndafu festival na maandalizi ya mbio hizo yataanza mapema.

Sauti ya Mbunge wa Rombo na Waziri wa elimu sayansi na teknolojia hapa nchini Profesa Adolf Mkenda.

Miongoni mwa washiriki wa mbio hizo  Segule Segule ambae ni Mkurugenzi wa bodi ya maji  bonde la pangani amesema kuwa wameshiriki katika mbio hizo zilizoratibiwa na wadau wa wilaya hiyo wakiongozwa na Mbunge wa Rombo amesema kuwa eneo hilo limewavutia kwa kuwa ni eneo wanalolifanyia kazi  na wao kama  Bodi ya maji bonde la Pangani wameshiriki katika mashindano hayo zaidi ya watu ishirini ili kuunga mkono watu wa Rombo kwa sababu wanaamini jambo hilo ni zuri kwani wanaimarisha afya na kupatikana fedha kwa ajili ya maendeleo ya kijamii lakini pia dhana ya utunzaji wa mazingira kwani mazingira yakitunzwa na vyanzo vya maji navyo vinatunzwa.

Sauti ya Mkurugenzi wa bodi ya maji bonde la Pangani Segule Segule.

Joel Naasi mmoja wa washiriki ambaye ni muhifadhi mkuu wa msitu wa kupandwa  wa Rongai amesema kufanyika kwa mbio hizo katika msitu huo ni katika kuunga mkono jitihada za mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika filamu aliyoizindua ya Royal Tour ambapo amesema kwa mbio hizo zililizofanyika watu wameweza kuona utunzaji wa mazingira  na kuweza kujikita katika utunzaji wa mazingira.

Hata hivyo amemshukuru mbunge wa jimbo hilo kwa kuunga mkono juhudi za mbio hizo na kupenda mashindano hayo yafanyikie kwenye msitu wa hifadhi ambapo amesema watu walioshiriki mbio hizo wataendelea kupata elimu itakayowasaidia kufanya mazingira yawe salama.

Sauti ya muhifadhi mkuu wa msitu wa kupandwa wa Rongai Joel Naasi.