Boma Hai FM

Saashisha ashiriki siku ya wanawake duniani, awaasa kuhusu mikopo

9 March 2024, 12:04 pm

Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe akuzungumza katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kata ya Narumu(picha na Edwin Lamtey)
Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe akitoa msaada kwa wenye uhitaji (picha na Edwin Lamtey)

Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe amewataka baadhi ya wanawake wanaokopa mikopo katika taasisi mbalimbali kuacha mara moja kwani mikopo hiyo inaleta athari kwa familia pamoja na jamii.

Na Edwin Lamtey

Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe amewaasa wananchi wa jimbo hilo hususani wanawake kuacha tabia ya kukopa katika taasisi zisizo rasmi na  zenye riba kubwa kitendo kinachowafanya kushindwa kurejesha na wengine kuzikimbia familia zao sababu ya marejesho.

Akizungumza katika maadhimisho ya kilele cha siku ya wanawake ambapo kiwilaya yamefanyika katika kata ya Narumu, Saashisha amesema kuwa kero ya mikopo hiyo kwa baadhi ya wanawake inatokana na baadhi yao kutowashirikisha waume zao wakati wa ukopaji.

“Leo mnasherekea siku hii ya wanawake na kupitia risala yenu mliyoisoma hapa nimesikia suala la mikopo; mikopo hii wengi wenu mnaiita kausha damu na ni kausha damu kweli kweli maana wengi wenu hamshirikishi waume zenu hata inafikia watu wanakuja kubeba vitanda nyumbani ndipo wanaume wanashtuka, haipendezi kopeni kwenye taasisi zinazoeleweka”. Alisema Saashisha.

Sanjari na hayo pia amewaasa wananchi kukemea vitendo vya ukatili vinavyoshamiri kwenye jamii, huku akisema kuwa vitendo hivi vinatokana na kuporomoka kwa maadili.

“Tumieni muda mwingi kuzungumza na watoto wenu, wakagueni watoto wenu maana vitendo vya ulawiti na ukatili wa kila aina vinazidi kushamiri na wakati mwingine viongozi wetu wa dini mtusaidie kukemea vitendo hivi katika nyumba zetu za ibada”.

Sanjari na hayo Saashisha Mafuwe hakusita pia kuzungumzia miradi ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Makowa – Mferejini ambapo ujenzi wake unaendelea.

Awali akizungumza katika maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya Hai Bi. Happyness Eliufoo amemshukuru mbunge Saashisha mafuwe kwa jinsi anavyosaidia wanawake wa wilaya ya Hai katika mapambano ya kujiinua kiuchumia huku akisema kuwa miradi inayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan imemrahishia mwanamke katika kujikwamua kiuchumi.

Katika maadhimisho hayo lilizinduliwa jukwaa la wanawake kwa ngazi ya kata zote huku ngazi ya wilaya Bi. Etropia Asenga akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa jukwaa hilo.