Boma Hai FM

Wanne wafariki dunia kwa madai ya matumizi ya dawa za kienyeji

11 July 2026, 2:31 pm

Pichani ni Majeneza yenye miili ya watu wa familia moja waliofariki kwa kunywa dawa za kienyeji pamoja na waombolezaji (Picha na Annasta Urio)

Watu wanne wa familia moja wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wafariki dunia katika mazingira yakutatanisha kwa madai ya kunywa dawa za kienyeji.

Na Annasta Urio, Hai-Kilimanjaro

Hali ya simanzi na taharuki imetanda katika familia ya Rasida Kimaro iliyopo kijiji cha Kimashuku, Kata ya Mnadani, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro baada ya watu wanne wa familia moja kufariki dunia katika mazingira yanayotajwa kuwa ya kutatanisha, huku mmoja akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC kwa madai ya kutumia dawa za kienyeji.

Ndugu, jamaa na majirani wa familia hiyo imekusanyika Julai 9, 2026 nyumbani kwa marehemu katika kijiji cha Kimashuku kwa ajili ya shughuli za maombolezo na kuhifadhi miili ya wapendwa wao waliopoteza maisha.

Marehemu hao ni Ismail Uronu (38), Judith Uronu (37), Rose Kweka (26) na Robson Mwema (34), ambao walifariki Kati ya Julai Julai 5 na Julai 8, 2026 katika tukio linalodaiwa kuhusishwa na matumizi ya dawa za kienyeji. Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi linamshikilia Beatrice Gabriel (59) kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Akizungumza msibani hapo, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Hai, Bryson Munisi amesema Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe, amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa na ameahidi kuendelea kuwa pamoja na familia katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Sauti ya katibu wa mbunge wa jimbo la Hai Brayson Munisi

Aidha Braysoni ameeleza kuwa Saashisha ameshiriki kikamilifu katika kufanikisha mazishi hayo kwa Hali kwa Mali na kwamba amewataka wananchi wa Kata ya Mnadani kushirikiana katika kuwalea watoto walioachwa na marehemu ili waweze kukua katika mazingira salama na yenye malezi bora.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mnadani, Emanuel Mgonja, amesema msiba huo ni pigo kubwa kwa kata hiyo na kuwataka wananchi kuendelea kushikamana, kusaidiana na kuifariji familia iliyoathirika.

Sauti ya diwani wa kata ya Mnadani Mhe. Emanuel Mgonja

Baadhi ya ndugu wa karibu wa marehemu walieleza kuwa vifo hivyo vilitokea ghafla na katika mazingira yasiyo ya kawaida, wakidai kuwa marehemu hawakuwa na historia ya kuugua kabla ya kuanza kuzidiwa kwa nyakati tofauti ndani ya kipindi kifupi.

Kwa mujibu wa maelezo yao, mwanzo walizidiwa mke na mume, baadaye Ismail Uronu naye akazidiwa, huku siku iliyofuata Rose Kweka naye akiugua na hatimaye kufariki dunia na kwamba Ndugu mwingine wa familia hiyo bado anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini

Sauti za Ndugu wa marehemu waliofikwa na msiba

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kimashuku ameiomba Serikali pamoja na wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia watoto walioachwa na marehemu, akieleza kuwa miongoni mwao yupo mtoto mwenye umri wa miezi saba huku familia ikiwa haina uwezo wa kuwahudumia ipasavyo.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Mnadani, Sembuli Mkilaa, ametoa wito kwa wananchi wa kata hiyo na jamii kwa ujumla kuepuka matumizi ya dawa na vinywaji ambavyo havijathibitishwa na mamlaka husika ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika.

Sauti ya Mtendaji wa Kata ya Mnadani, Sembuli Mkilaa,

Pichani ni Viongozi wa Kata ya Mnadani pamoja na waombolezaji wengine wakati wa mazishi ya watu wanne wa familia moja (Picha na Annasta Urio)

Akizungumza na Redio Boma Hai FM, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema kuwa uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo.