Boma Hai FM

Masama Magharibi yaandika historia mpya ya elimu, kujenga sekondari mpya

27 June 2026, 9:58 am

Pichani ni afisa elimu msingi halmashauri  wilaya ya Hai Musa Kalanje (picha na Annasta Urio)

Wananchi wa Masama Magharibi wamehimizwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mashua kwa kulinda mradi, kutoa nguvu kazi na kutunza vifaa vya ujenzi, huku wakieleza matumaini kuwa shule hiyo itapunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.

Na Anasta Urio

Hai- Kilimanjaro

Wananchi wa Kata ya Masama Mashariki wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kulinda, kusimamia na kutunza fedha za ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari ya Mashua, unaogharimu zaidi ya shilingi milioni 584 zilizotolewa na Serikali.

Wito huo umetolewa  Juni 25,2026 na Diwani wa Kata ya Masama Magharibi Eliufoo Christopher, wakati wa uzinduzi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi 584,280,029.

Pichani ni na Diwani wa Kata ya Masama Mashariki Eliufoo Christopher akizungumza na wananchi(picha na Anasta Urio)

Eliufoo  ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuikumbuka kata hiyo, akibainisha kuwa kwa muda mrefu wanafunzi walilazimika kusafiri umbali wa takribani kilomita tisa kufuata masomo katika Shule ya Sekondari Bwani. Pia amesisitiza umuhimu wa kupanda miti katika eneo la shule ili kuhifadhi mazingira.

Sauti ya diwani wa kata ya Masama Magharibi Eliufoo Christopher

Naye Afisa Elimu Msingi Halmashauri  wilaya ya Hai Musa Kalanje, amempongeza Diwani Eliufoo Christopher kwa juhudi zake za kuisemea kata hiyo na kwamba serikali imejipanga kuboresha mazingira ya kujifunzia ili kuendana na mfumo mpya wa elimu unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka 2028.

Sauti ya afisa elimu msingi halmashauri  wilaya ya Hai Musa Kalanje

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Emanuel Marco, amewataka wananchi wa Masama Mashariki kujitokeza kwa wingi kushiriki ujenzi huo kwa kutoa nguvu kazi, pamoja na kulinda vifaa na pembejeo za ujenzi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo wameeleza kufurahishwa na ujio wa mradi huo, wakiahidi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake huku wakimshuru  Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe, kwa juhudi zake za kuisemea kata hiyo hadi kufanikisha upatikanaji wa shule hiyo, ambayo inatarajiwa kupunguza adha ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu kutafuta elimu.

Pichani ni wananchi wa kata ya Masama Magharibi waliojitokeza kwa ajili ya kupokea mradi huo( picha na Anasta Urio)