Boma Hai FM
Boma Hai FM
10 August 2026, 9:19 am

Madiwani na wataalamu mbalimbali wa wilaya ya Hai wametembelea mabanda ya maonyesho nanenane yaliyopo katika viwanja vya Themi Jijini Arusha kujifunza na kujionea mbinu bora za kilimo na bidhaa za kilimo
Na Oliver Joel, Njiro-Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Mheshimiwa Hassan Bomboko, ametembelea mabanda mbalimbali katika maonesho ya 32 ya Kilimo, Mifugo katika Sherehe za Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Themi Njiro jijini Arusha.
Mheshimiwa Bomboko ametembelea banda la halmashauri ya wilaya ya Hai agosti 6 2026 ambapo amepongeza tafiti na bunifu mbalimbali zinazofanywa na taasisi mbalimbali huku akitoa wito kwa wakulima na wafugaji walioshiriki maonesho hayo kuchukua mbinu mbalimbali za ufugaji na ukulima zitakazowawezesha kuboresha shughuli zao.
Hata hivyo mheshimiwa Bomboko amewapongeza waandaaji wa maadhimisho ya nanenane na kuongeza kuwa mwitikio wa wananchi kujitokeza katika maadhimisho haya ni mkubwa ukilinganishwa na miaka iliyopita ,hivyo kuwataka wananchi wa Hai ambao ni wakulima na wafugaji kutobaki nyuma kushiriki katika maadhimisho hayo.

Aidha Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka ambaye pia ni diwani wa kata ya Muungano ameambatana na madiwani wa wilaya Hai kutembeleamaonesho ya 32 ya Kilimo mifugo katika Sherehe za nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Themi Njiro, Arusha.
Akizungumza agosti 7 2026 mara baada ya kutembelea banda la halmashauri ya wilaya ya Hai na mabanda mengine,mwenyekiti wa halmashauri amesema kuwa mbinu za kisasa walizojifunza zitawawezesha madiwani kufikisha mbinu hizo za kilimo na ufugaji kwa wananchi katika kata zao.
Naye Ruth Lyamuya ambaye ni mkurugenzi wa Shalom products wanaojihusisha na usindikaji wa viungo vya chakula,viungo vya chai na tiba lishe ambaye amepeleka bidhaa katika maonesho hayo ameishukuru halmashauri ya wilaya ya Hai kwa kuwawezesha kupata nafasi ya kutangaza bidhaa zao katika maonesho hayo.