Boma Hai FM

Polisi Hai watoa elimu kupinga uhalifu

27 August 2026, 9:17 am

Pichani ni Polisi Jamii wilaya ya Hai wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari Lyamungo (Picha na Henry Keto)

Jeshi la Polisi wilaya ya Hai kitengo cha Polisi jamii limetoa elimu kuhusu kupinga uhalifu na matumizi ya madawa ya kulevya katika shule ya sekondari Lyamungo na katika jamii.

Na Henry Keto

Jeshi la Polisi Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, kupitia Kitengo cha Polisi Jamii, limetoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lyamungo kuhusu madhara ya vitendo vya kihalifu, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na umuhimu wa kuzingatia nidhamu ya msomo shuleni.

‎Elimu hiyo imetolewa Agosti 24, 2026, katika Shule ya Sekondari Lyamungo, ambapo mkuu wa Polisi Wilaya ya Hai, OCD SSP Suzan Kidiku, amewataka wanafunzi kuachana na vitendo vyote vya kihalifu na matumizi ya dawa za kulevya, akisisitiza umuhimu wa kulinda mustakabali wao.

‎SSP Suzan Kidiku amesema matumizi ya dawa za kulevya pamoja na utovu wa nidhamu vinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa ufaulu wa mwanafunzi na uwezo wake wa kujifunza. Aidha, ameeleza kuwa baadhi ya vitendo hivyo vinaweza kuwa kikwazo kwa vijana kupata fursa mbalimbali za ajira na maendeleo baada ya kumaliza masomo.

Sauti ya SSP Hai wilaya ya Hai OCD Suzan Kidiku
Pichani ni Afande OCD SSP Suzan Kidiku (Kulia) na Mkuu wa Polisi Jamii wilaya ya Hai SP Elishafra (kushoto) pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari lyamungo (Picha na Henry Keto)

Ametoa wito kwa wanafunzi hao kutumia fursa waliyonayo ya kupata elimu kwa kujituma katika masomo, kuwa na nidhamu na kuepuka makundi au vitendo vinavyoweza kuharibu maisha yao, ili waweze kujenga uwezo na kufikia ndoto zao hapo baadaye.

Sauti ya Mkuu wa polisi Jamii Wilaya ya Hai SP Elishafra

Nao wanafunzi wa shule ya sekondari lyamungo wameshukuru ujio wa polisi hao katika shule yao, kwani imewapa hamasa ya kusima kwa bidii ili kutimiza ndoto zao, pamoja na kuahidi kulinda amani ya nchi na pamoja na kuepuka matumizi ya madawa ya kulevya

Sauti ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Lyamungo
Pichani ni mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Hai SP Elishafra akizungumza na wanafunzi juu ya umuhimu wakutia bidii kwenye masomo (Picha na Henry Keto)