Boma Hai FM

Siha yatakiwa kutozalisha madeni mapya,wanaodai kulipwa

24 August 2026, 6:40 pm

Pichani ni Dankan Urassa mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Siha (katikati) makamu mwenyekiti wa halhashauri Stanley Nkini (wa kwanza kushoto) pamoja na kaimu mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya Siha Marco Masue (picha na Elizabeth Mafie)

Halmashauri ya Wilaya ya Siha imetakiwa kusimamia kwa umakini utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia uwezo wa kifedha ili kuepusha kuzalisha madeni mapya, huku ikiendelea kulipa madeni yaliyopo.

Na Elizabeth Mafie

Siha – Kilimanjaro

Halmashauri ya wilaya ya Siha  mkoani Kilimanjaro imetakiwa kutokuzalisha madeni mapya kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku ikiendelea kuchukua hatua za kulipa madeni yaliyopo, yakiwemo yanayodaiwa na watumishi.

Wito huo umetolewa Agosti  24, 2026 na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Siha Dankan  Urassa , wakati wa mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri.

Urassa amesema ni muhimu kwa halmashauri kupanga miradi kulingana na uwezo wake wa kifedha na kuhakikisha fedha zinazosimamiwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuepuka kuanzisha miradi isiyokuwa na uhakika wa fedha na hatimaye kuacha madeni mapya.

Sauti ya mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Siha Dankan Urassa.

Amesema usimamizi madhubuti wa miradi na matumizi ya fedha kwa kuzingatia bajeti ni sehemu muhimu ya kulinda mapato ya halmashauri na kuhakikisha fedha zinazoelekezwa kwenye maendeleo zinatumika kwa ufanisi.

Pichani ni madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Siha( picha na Elizabeth Mafie)

Kwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Siha DKt Christopher Timbuka amesema tatizo la madeni ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji usimamizi wa karibu, akiwataka watumishi kutekeleza majukumu yao kwa wakati, kuheshimu ratiba za kazi na kuwasilisha taarifa kwa wakati.

Dkt Timbuka amesema nidhamu katika utekelezaji wa majukumu na ufuatiliaji wa shughuli za halmashauri utasaidia kuboresha utendaji na kupunguza changamoto zinazotokana na madeni.

Wakati huo huo, Dkt Timbuka amewataka madiwani kushirikiana na viongozi wa serikali kuhamasisha wananchi kuhakikisha watoto wenye umri unaolengwa wanapatiwa chanjo ya polio katika kampeni itakayofanyika kuanzia Agosti  27 hadi 30 mwaka huu.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Siha Dkt Christopher Timbuka.

Amesema ushiriki wa viongozi na jamii ni muhimu katika kuhakikisha watoto wote wanaostahili wanapata chanjo hiyo.

Nao baadhi ya madiwani walioshiriki mkutano huo wameitaka halmashauri kuendelea kusimamia kwa karibu maamuzi ya baraza, matumizi ya fedha na utekelezaji wa miradi, ili kudhibiti ongezeko la madeni na kuhakikisha rasilimali za halmashauri zinatumika kwa manufaa ya wananchi.

Pichani ni wataalamu mbalimbali wa halmashauri ya wilaya ya Siha (picha na Elizabeth Mafie)