Boma Hai FM
Boma Hai FM
29 September 2026, 6:20 pm

Na Elizabeth Mafie
Jukumu la kulinda haki na kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki na za kisheria si jukumu la taasisi moja pekee, bali ni la serikali, mahakama, jeshi la polisi, asasi za kiraia, viongozi wa dini na wazee wa kimila.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 29, 2026 na kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Marko Masue, katika ukumbi wa Angaza Women Center uliopo wilayani Siha wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la mazingira na haki za binadamu(Envirocare) yaliyohudhuriwa na watu 51 kutoka katika makundi mbalimbali.
Marko Masue amewasihi viongozi wa dini pamoja na wazee wa kimila kutumia nafasi zao katika jamii kuhamasisha haki, amani, hekima, sheria na kulinda utu wa kila mwananchi na kwamba watendaji wa kata wanapaswa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kuelekezwa kwenye mifumo sahihi ya kutatua migogoro yao.

Ameongeza kuwa jeshi la polisi, mahakama na taasisi nyingine za haki ni muhimu kuendelea kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwa haki, heshima na kuzingatia sheria huku akihimiza wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutumia fursa ya mafunzo hayo kujifunza, kuuliza maswali na kushiriki kikamilifu katika masuala yanayohusu haki zao.

Naye mkurugenzi wa miradi wa shirika hilo, Amosi Mbwambo, amesema mradi huo ni wa miaka mitatu ambao umeanza rasmi mwaka 2026 hadi 2028, ukiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu masuala ya mazingira ,haki za binadamu , na eneo la jinsia hususani masuala ya mirathi, pamoja na kuboresha maisha ya wananchi wa Siha.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo mtendaji wa Kata ya Livishi, Subela Saidi, na Honest Asei, mtendaji wa Kata ya Karansi, wamesema mafunzo hayo waliyopatiwa na shirika la Envirocare yatawasaidia katika kutatua migogoro mbalimbali, ikiwemo migogoro ya ardhi, pamoja na kuwaelimisha wananchi wao kuhusu haki za binadamu.
Envirocare ni asasi isiyokuwa ya kiserikali iliyoanzishwa mwaka 1993, makao makuu yakiwa mkoani Dar es Salaam pamoja na ofisi ndogo zinazopatikana mkoani Kilimanjaro, wilaya ya Siha na Shirika hilo linafanya kazi katika maeneo makubwa matatu ambayo ni mazingira, haki za binadamu na jinsia