Boma Hai FM
Boma Hai FM
23 September 2026, 10:06 am

Katika kuhakikisha sherehe na mikusanyiko mbalimbali inafanyika kwa usalama na kuzingatia taratibu, Halmashauri ya Wilaya ya Hai imewataka waandaaji kutoa taarifa mapema na kuhakikisha wanapata vibali kabla ya shughuli hizo kuanza.
Na Juma Robert
Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Stanley Kiduko, amewataka wananchi wanaotarajia kufanya sherehe na mikusanyiko mbalimbali kuhakikisha wanapata vibali kabla ya kuendesha shughuli hizo.
Kiduko ametoa kauli hiyo Septemba 22 2026, wakati akizungumza na Radio Boma Hai FM, ambapo amesema utaratibu huo unahusu shughuli mbalimbali ikiwemo harusi, kitchen party, send-off, graduation, mikusanyiko na matamasha yanayohusisha idadi kubwa ya watu.
Amesema vibali hivyo vinaisaidia Halmashauri kufahamu shughuli zinazofanyika katika maeneo yake na kuhakikisha zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria, taratibu, usalama, maadili pamoja na mila na desturi za jamii.
Aidha Kiduko amesema baadhi ya sherehe hufanyika katika kumbi ambazo hazijulikani na Halmashauri, hali inayosababisha changamoto katika ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli hizo.
Amewataka wananchi na wamiliki wa kumbi kushirikiana na Halmashauri kwa kutoa taarifa mapema na kuhakikisha vibali vinapatikana kabla ya shughuli kuanza, ili sherehe na mikusanyiko hiyo ifanyike kwa utulivu, usalama na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.