Boma Hai FM

Kamati ya fedha Hai yahimiza jamii kuchangia miradi ya maendeleo

30 July 2026, 2:51 pm

Pichani ni mwenyekiti wa kamati ya fedha,uchumi na mipango ambae pia ni mwenyekiti Halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka (aliyevaa kofia)kaimu afisa ardhi wilaya ya Hai Clement Mgullu pamoja na wajumbe wa kamati hiyo ambao ni madiwa wa halmashauri ya wilaya ya Hai wakitazama ramani ya maeneo yanayomilikiwa na halmashauri(picha na Riziki Lesuya)

Kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Hai imehimiza ushiriki wa wazawa na wadau wa maendeleo katika kuchangia utekelezaji wa miradi ya kijamii, huku pia ikisisitiza umuhimu wa kulinda maeneo ya umma kwa kuyapima na kuyapatia hati za ardhi ili kuzuia uvamizi na migogoro.

Na Elizabeth Mafie

Hai – Kilimanjaro

Wadau wa maendeleo pamoja na wazawa wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kushirikiana na Serikali kwa kujitolea kuchangia ujenzi wa shule, zahanati na miundombinu ya barabara ili kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.

Wito huo umetolewa Julai 29, 2026 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango, Edmund Rutaraka, wakati akihitimisha ziara ya siku mbili ya kamati hiyo ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Hai.

Pichani ni wajumbe wa kamati ya fedha,uchumi na mipango ambao pia ni madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Hai wakiingia katika kivutio cha utalii Chemka Hot Spring (picha na Riziki Lesuya)

Katika siku ya mwisho ya ziara hiyo, kamati imetembelea miradi mbalimbali ikiwemo kivutio cha utalii cha Chemka pamoja na maeneo yanayomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Hai, kwa lengo la kujionea utekelezaji wa miradi hiyo na huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Pichani ni afisa maliasili wilaya ya Hai Mbayani Mollel akimuelezea jambo mwenyekiti wa kamati ya fedha ,uchumi na mipago Edmund Rutaraka(picha na Riziki Lesuya)

Akizungumzia ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Losaa, Rutaraka amesema mradi huo unatekelezwa kwa ufadhili wa mdau wa maendeleo ambaye ni mzawa wa kijiji hicho huku akiwataka  wadau wengine pamoja na wazawa kuiga mfano huo kwa kujitolea kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Sauti ya mwenyekiti wa kamati ya fedha,uchumi na mipango na mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka.

Aidha amesema kamati hiyo imemwelekeza Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Hai kuhakikisha maeneo yote yanayomilikiwa na halmashauri yanapatiwa hati ili yawe salama na kuepeuka uvamizi wa wananchi.

Pichani ni mwenyekiti wa kamati ya fedha ,uchumi na mipango ambae pia ni mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Hai Edmundi Rutaraka (aliyevaa kofia)mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Hai Dionis Myinga(wa kwanza kulia) pamoja na wataalamu mbalimbali wa halmashauri ya wilaya ya Hai wakiwa katika kivutio cha utalii Chemka Hot Spring (picha na Riziki Lesuya)

Kwa upande wake kaimu afisa ardhi  wa wilaya  ya Hai  Clement Mgullu amesema ni muhimu Halmashauri na Serikali kuhakikisha maeneo yote inayoyamiliki yanapata hati za ardhi ili kuzuia migogoro isiyo ya lazima kati ya Serikali na wananchi, pamoja na kulinda maeneo ya umma dhidi ya uvamizi.

Sauti ya kaimu afisa ardhi wilaya ya Hai Clement Mgullu.