Boma Hai FM
Boma Hai FM
25 September 2026, 5:00 pm

LATRA isimamie kikamilifu nauli za daladala na Costa ili kuwaepusha wananchi na ongezeko holela la nauli.” — Hassan Bomboko, Mkuu wa Wilaya ya Hai.
Na Annasta Urio
Mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko, ameitaka mamlaka ya udhibiti usafiri ardhini (LATRA) mkoa wa Kilimanjaro kusimamia kikamilifu nauli za daladala na magari ya abiria aina ya Costa, ili kuwaepusha wananchi na ongezeko holela la nauli.
Bomboko ametoa agizo hilo wakati akizungumza katika kikao cha baraza la wafanyabiashara kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
Sambamba na hilo amewataka LATRA kusimamia Vituo halali vya daladala pamoja na kudhibiti idadi ya wasafiri katika vyombo vya umma ili kuepuka ajali.

Naye meneja wa LATRA mkoa wa Kilimanjaro Subira Valerian amesema mamlaka hiyo imeendelea kusimamia utoaji wa vibali vya biashara pamoja na nauli za usafiri wa umma, huku akisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya madereva watakaobainika kutoza nauli zaidi ya kiwango kilichowekwa.
Kwa upande wake mkuu wa polisi wilaya ya Hai SSP Suzan Kidiku amesema TANROADS pia wanapaswa kuzingatia zaidi mazingira na usalama wa maeneo kabla ya kutoa vibali vya biashara, akitolea mfano eneo la kona ya barabara ya Sanya ambalo amesema linaweza kuhatarisha usalama wa wananchi.