Boma Hai FM
Boma Hai FM
14 September 2026, 11:47 am

Watumishi wawili wa Halmashauri ya Siha wamefukuzwa kazi baada ya kubainika kutoroka kazini kwa siku 104 na 156, huku watumishi wengine wanne wakipelekwa kwenye matibabu ya uraibu kwa kipindi cha miezi mitatu kutokana na matumizi ya pombe kupita kiasi.
Na Bahati Chume
Siha – Kilimanjaro
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro limewafukuza kazi watumishi wawili kwa tuhuma za utoro kazini, huku watumishi wengine wanne wakipelekwa katika kituo maalumu cha matibabu ya uraibu baada ya kubainika kutumia pombe kupita kiasi.
Hatua hizo zimechukuliwa baada ya Baraza hilo kupitia mashauri ya kinidhamu dhidi ya watumishi hao na kubaini ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Halmashauri hiyo katika kikao cha kawaida cha Baraza kilichofanyika Septemba 8, 2026, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Siha, Duncan Urassa, amesema watumishi waliofukuzwa kazi ni Muuguzi Daraja la Kwanza wa Hospitali ya Wilaya, Vitalis Bajuta, aliyebainika kutoroka kazini kwa siku 104, pamoja na Mtendaji wa Kijiji cha Lawate, Joel Mulenga, aliyebainika kutokuwepo kazini kwa siku 156.
Urassa amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 42 ya Watumishi wa Umma, mtumishi anayefanya utoro kazini kwa siku tano au zaidi anapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu, na kwamba baada ya taratibu zote kufuatwa, Baraza liliridhia watumishi hao kufukuzwa kazi.
Ameonya kuwa Halmashauri hiyo haitasita kuchukua hatua dhidi ya watumishi watakaokiuka wajibu wao, ikiwemo utoro, ulevi na ubadhirifu wa mali ya umma, akiwataka watumishi kuzingatia sheria na taratibu za utumishi wa umma ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

“Ni kweli hatutasita kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wote wazembe watakaokiuka wajibu wao, kwani wanarudisha nyuma jitihada za kuwaletea maendeleo wananchi. Hatutawavumilia,” amesema Urassa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Hellen Mwambeta, amesema kabla ya uamuzi wa kuwafukuza kazi, Halmashauri ilichukua hatua mbalimbali za kinidhamu, ikiwemo kuwaita katika vikao, kuwaeleza na kuwashauri kuhusu wajibu wao, lakini utoro uliendelea.
Akizungumzia watumishi wanne waliobainika kutumia pombe kupita kiasi, Mwambeta amesema wamepelekwa katika kituo maalumu cha matibabu ya uraibu kwa kipindi cha miezi mitatu.
Amesema gharama za matibabu ya watumishi hao zinagharamiwa kwa ushirikiano kati ya Halmashauri na wazazi wa watumishi hao.