Boma Hai FM
Boma Hai FM
26 August 2026, 4:48 pm

Wazazi na walezi watakiwa kushiriki kikamilifu katika kampeni ya chanjo ya polio kwa kuhakikisha watoto walio chini ya umri wa miaka 10 wanapata chanjo hiyo, ikiwa ni hatua ya kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa polio.
Na Vaileth Silvester
Hai, Kilimanjaro
Afisa Afya na mratibu wa elimu ya afya kwa jamii wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro George Masawe, amewataka wazazi na walezi wenye watoto walio chini ya umri wa miaka 10 kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kupata chanjo ya polio ya matone, katika kampeni inayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2026.
Akizungumza katika kipindi cha siku mpya kinachorushwa na Radio Boma Hai Fm Agosti 22, 2026 Masawe amesema kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha kinga kwa watoto dhidi ya ugonjwa wa polio, pamoja na kuzuia uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa huo katika jamii.
Amesema ushirikiano wa wazazi na walezi ni muhimu katika kufanikisha kampeni hiyo, huku akiwataka kutowazuia watoto wao kupata chanjo hiyo ili waweze kupata ulinzi unaohitajika dhidi ya polio.
Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Wilaya ya Hai, Fortunatus Kisheo, amesema chanjo hiyo ni salama kwa watoto na amewataka wazazi na walezi kutokuwa na hofu wakati wa kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo.
Amesema chanjo hiyo ni muhimu katika kuongeza ulinzi wa watoto dhidi ya polio na kuimarisha hatua za afya ya jamii katika kuzuia ugonjwa huo.
Kampeni hiyo inatarajiwa kuanza Agosti 27 saa 1:30 asubuhi na kuendelea hadi Agosti 30, 2026, huku wazazi na walezi wakihimizwa kutumia fursa hiyo kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo.
