Boma Hai FM
Boma Hai FM
6 June 2025, 12:30 am

Maadhimisho ya kilele cha wiki ya Mazingira Duniani ambayo kwa mkoa wa kilimanjaro yamefanyika wilaya ya Hai
Na Henry Keto,Hai-Kilimanjaro
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu ametoa wito kwa Wananchi kupanda miti na kuitunza na kuhakikisha mazingira yanakuwa safi Wakati wote.
Akizungumza wakati wa hotuba yake kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani ambapo katika Mkoa wa Kilimanjaro yamefanyika wilaya ya Hai, amewaasa Wananchi kurudisha uoto wa asili kama ilivyokuwa miaka ya 1980’s-1990’s.
Ametoa maagizo kwa Mkuu wa Wilaya kuhakikisha miti iliyopandwa inakua vizuri,ilindwe isiliwe na mifugo, ambapo pia amemtaka kutumia Sheria kwa Mifugo itakayokula miti ichukuliwe na kutaifishwa na Serikali, aidha amemtaka mkurugenzi mtendaji kuhakikisha wanapopima viwanja kabla mtu hajajenga ahakikishe amepanda miti mitano.
Mkuu wa wilaya ya hai Hassan bomboko amesema katika maadhimisho ya wiki ya kilele cha Mazingira Duniani wilaya ya Hai umepanda jumla ya Miti elfu moja,na umeweka mikakati thabiti yakuitunza Miti isiliwe na mifugo.
Pia amesema wameweka utaratibu wa kila jumamosi ya mwisho wa mwezi kutakuwa ni siku rasmi yakufanya usafi katika maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Hai.

Nae mkuu wa wilaya ya Rombo Raymond Mangwala ametoa salamu za Wananchi wa rombo ambapo amesema katika Wilaya ya Rombo wamefanya usafi na kuchoma taka zote zikiwemo taka za plastic na kuhakikisha wilaya ya Rombo inaendelea kuwa katika hali ya usafi wakati wote.
Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Edmund Rutaraka amesema kuanzia kipindi cha mwaka 2021/2022 mpaka Sasa uoteshaji wa miti kwa wilaya ya Hai umefikia asilimia 91, mbali na changamoto zinazotokana na mtindo wa maisha ya binadamu ambao ni wakulima na wafugaji pamoja na mabadiliko ya Hali ya hewa lakini Bado juhudi za kuhakikisha wilaya inakuwa na Mazingira mazuri na yakuvutia.