Boma Hai FM
Boma Hai FM
21 May 2026, 12:48 pm

Kutokana na kuibuka kwa wimbi la watoa elimu ya lishe mtandaoni wasio na taaluma husika,mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe ahoji ni ni lini sheria itaanza kutekelezwa kikamilifu kwa wote wanaokiuka utaratibu huo.
Na James Gasindi
Dodoma
Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro Saashisha Mafuwe amehoji Serikali kuhusu ongezeko la watu wanaotoa elimu na ushauri wa lishe kupitia mitandao ya kijamii bila kuwa na taaluma zinazotambulika, hali inayoweza kuhatarisha afya za wananchi na kuleta upotoshaji katika jamii.
Akiuliza Swali kwa wizara ya Afya Mei 20, 2026 Saashisha amesema tayari serikali imekiri kuwepo kwa tatizo hilo pamoja na uwepo wa sheria ya afya ya jamii ya mwaka 2009 kifungu cha 173 kinachomtaka mtu anayetoa maudhui ya afya kupata kibali rasmi kutoka kwa mamlaka husika na kuuliza Je ni lini sheria hiyo itaanza kutekelezwa kikamilifu kwa wote wanaokiuka utaratibu huo.
Saashisha pia amehoji ni lini Serikali itaanza kuwatumia maafisa lishe walioajiriwa katika wilaya mbalimbali nchini kutoa elimu kwa wananchi Pamoja na kuunda baraza la lishe Tanzania ili wananchi wawe wanapata elimu kutoka kwa wataalamu wenye sifa badala ya watu wasio na taaluma ya afya.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya Dkt Florence Samizi amesema Serikali tayari imeanza kufanya tathmini maalum itakayosaidia kuwatambua watu wanaotoa taarifa za afya bila vibali, kuweka kanuni na taratibu za utoaji wa vibali pamoja na kuunda kamati ya kufuatilia maudhui hayo.
Dkt. Samizi amesema Serikali ina zaidi ya maafisa lishe 600 nchini na kuwataka wataalamu hao kutumia zaidi mitandao ya kijamii pamoja na redio za kijamii kuwafikia wananchi wengi, huku akiitaka jamii kuhakikisha inapokea taarifa za afya kutoka kwenye vyanzo rasmi na wataalamu wenye taaluma zinazotambulika.