Boma Hai FM
Boma Hai FM
23 June 2026, 11:27 am

Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka, amesema serikali na vyombo vya ulinzi vilichukua hatua mbalimbali kudhibiti sintofahamu zilizojitokeza wakati wa mazishi ya kijana Emanueli, ikiwemo kuwaachilia waliokamatwa na kutumia nguvu kiasi kurejesha utulivu na kwamba mazishi yalikamilika salama na hadi sasa hali ya usalama katika Wilaya ya Siha imeendelea kuwa shwari.
Na James Gasindi
Siha- Kilimanjaro
Kutokana na sintofahamu iliyojitokeza wakati wa mazishi ya kijana Emanueli aliyefariki dunia baada ya kupata ajali ya pikipiki katika Wilaya ya Rombo, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka, ameeleza hatua zilizochukuliwa na mamlaka za serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti hali hiyo na kuhakikisha amani inaendelea kuwepo katika wilaya ya Siha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Julai 17, 2026, Dkt. Timbuka amesema marehemu alipata ajali Juni 12, 2026 baada ya pikipiki aliyokuwa akiendesha kugongana na gari la Polisi wakati wa operesheni ya ukaguzi, ambapo ilidhaniwa kuwa ilikuwa imebeba bidhaa haramu zikiwemo mirungi au bangi.
Amesema siku ya mazishi kundi kubwa la waendesha bodaboda lilielekea Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC kuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya kuusafirisha hadi Siha na kwamba Jeshi la Polisi liliwashauri kutofanya msafara mkubwa wa pikipiki ambao ungeweza kuathiri matumizi ya Barabara Kuu ya Moshi–Arusha, lakini baadhi yao walikaidi ushauri huo na kusababisha watu 10 kukamatwa huku wengine wakikusanyika Bomang’ombe kusubiri kuwasili kwa mwili huo.
Dkt. Timbuka amesema mwili ulipowasili Siha majira ya saa tisa alasiri, baadhi ya vijana walikataa kuendelea na mazishi wakitaka wenzao waliokamatwa waachiwe huru kabla ya shughuli za maziko kuendelea na Jeshi la Polisi liliwaachilia waliokuwa wamekamatwa kwa lengo la kudumisha amani, lakini baada ya kuachiliwa kundi hilo liliwasilisha madai mengine likitaka kufika eneo la tukio kabla ya mazishi kuendelea na baadaye baadhi yao waliweka jeneza juu ya gari la Mkuu wa Wilaya ili kuzuia viongozi kuondoka eneo hilo.
Ameongeza kuwa kutokana na viashiria vya hatari ya kiusalama, ikiwemo baadhi ya watu kuonekana kuwa na mawe na silaha ndogondogo pamoja na giza kuanza kuingia, Jeshi la Polisi lililazimika kutumia nguvu kiasi kurejesha utulivu na kuhakikisha mazishi yanaendelea na shughuli za mazishi hayo zilikamilika salama na kusisitiza kuwa tangu usiku wa tukio hilo hadi sasa hakuna tukio lolote la uvunjifu wa amani lililoripotiwa huku hali ya usalama katika Wilaya ya Siha ikiendelea kuwa shwari.