Boma Hai FM

Vyama vya ushirika Hai vyatakiwa kuwekeza uwekezaji wenye tija

15 April 2026, 2:44 pm

Pichani ni mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya uwekezaji na maeneo maalumu ya kiuchumi (TISEZA) Giliad Teri (anaezungumza)katikati ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka pamoja na mrajisi msaidizi mkoa wa Kilimanjaro Jackline Senziga(picha na Anasta Urio)

Ziara ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA) wilayani Hai imelenga kuhamasisha vyama vya ushirika kuwekeza kwa tija, kutafuta vyanzo mbadala vya kipato na kupata masoko ili kukabiliana na changamoto za tabia nchi na kuboresha maisha ya wakulima

Na Anasta Urio

Hai- Kilimanjaro

Vyama vya ushirika (AMCOS) wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro vimetakiwa kufanya uwekezaji wenye tija kwenye mashamba ya ushirika ili kunufaisha vyama na taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya uwekezaji na maeneo maalumu ya kiuchumi (TISEZA) Giliad Teri ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea, kutoa elimu na ushauri kwa vyama vya ushirika kufuatia  ombi lililotolewa na Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe.

 Teri ameeleza kuwa ili vyama vya ushirika viendelee  kuwa na uwekezaji wenye matokeo chanya kwa pande zote kwa mwekezaji na vyama vya ushirika ni lazima viwe na mbinu mbadala wa mapato ili kutatua changamoto za masoko na mabadiliko ya tabia nchi.

Sauti ya mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya uwekezaji na maeneo maalumu ya kiuchumi (TISEZA) Giliad Teri

Nae Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Kilimanjaro Jackline Senziga ameviasa vyama hivyo kutumia TISEZA kwa ufasaha katika kutafuta masoko ya mazao na bidhaa mbali mbali zinazotokana na ushirika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmshauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka ambaye katika ziara hiyo alimwakilisha Mbunge wa jimbo la Hai  amesema  ziara hiyo itasaidia vyama hivyo  na wawekezaji kupata elimu na uelewa wa fursa mbalimbali ambazo zipo kwenye mashamba ya ushirika pamoja na changamoto ambazo zinaweza kutatuliwa na bodi husika kama kuwekeza kwenye mazao tofauti na kahawa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kama ukame.

Sauti ya mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka

Nae Meneja wa kampuni ya uwekezaji ya APKL Donald Temba amemshukuru Mbunge kwa ziara hiyo na kuomba TISEZA iwasaidie kupata soko la uhakika (direct export) ili wakulima wa zao la kahawa wanufaike  na kupata hamasa zaidi ya kulima zao hilo.