Boma Hai FM
Boma Hai FM
21 July 2026, 7:03 pm

Wilaya ya Hai iliyopo Mkoani kilimanjaro imeimarisha utekelezaji wa utoaji wa huduma ya lishe bora kwa wananchi kwa kutoa Elimu ya lishe kupitia mikutano mbalimbali taasisi za Elimu na ufuatiliaji wa utoaji wa matone ya vitamini A kwa watoto.
Na Henry Keto, Hai-Kilimanjaro
Wazazi na walezi wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro wamehimizwa kuzingatia matumizi ya lishe bora, ikiwemo vyakula vilivyoongezwa virutubisho, ili kuboresha afya na kuimarisha kinga ya mwili kwa watoto.
Wito huo umetolewa na Afisa Lishe wa Wilaya ya Hai Domini Kimaro, wakati wa kikao maalumu cha wataalamu wa lishe wa wilaya hiyo kilichofanyika Julai 21, 2026, katika ukumbi wa mkuu wa wilaya ya Hai. Kikao hicho kilihusisha maafisa watendaji wa kata zote 17 ambao ni wajumbe wa kamati ya lishe, ambapo walitoa tathmini ya hali ya lishe katika maeneo yao.
Kimaro amesema hali ya utekelezaji wa afua za lishe wilayani Hai imeendelea kuimarika kutokana na utoaji wa elimu ya lishe kwa wananchi pamoja na ufuatiliaji wa shughuli mbalimbali za lishe katika jamii.
Akitoa tathmini ya kata yake Afisa Mtendaji wa Kata ya Mnadani, Sembuli Mkilaa, amesema hali ya lishe katika shule za msingi na sekondari imeimarika kwa zaidi ya asilimia 90, huku wanafunzi wengi wakipata chakula chenye lishe bora wakiwa shuleni.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa kata ya Kia Stanford Mwakalinga, amesema wananchi wa kata hiyo wameendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki mikutano ya elimu ya lishe, hatua ambayo imechangia kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa lishe bora huku akihamiza wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kueneza elimu hiyo kwenye jamii.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko kimeazimia kuongeza uzalishaji wa unga lishe kupitia mashine zilizopo kwenye kata mbalimbali na kusambaza unga huo katika shule zote za wilaya , aidha kikao kimependekeza kuimarisha utoaji wa elimu ya lishe kwa wazazi, walezi na wanafunzi ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa lishe bora.
Akihitimisha kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Hai amewaelekeza wajumbe wa kamati ya lishe kuhakikisha huduma za lishe zinaboreshwa katika maeneo yote ya wilaya, sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya lishe bora kwa ajili ya afya na ustawi wa jamii.