Boma Hai FM

Saashisha aiomba serikali kukalimisha zahanati, Foo, Uroki, Romu kunufaika

29 August 2026, 3:18 pm

Pichani ni mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe akiuliza swali bungeni (picha kwa msaada wa mtandao)

Mbunge wa Jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe, ameendelea kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wake, akiiomba Serikali kuunga mkono juhudi za wananchi waliokwisha anza ujenzi wa zahanati kwa michango yao, na kwamba kukamilika kwa zahanati hizo kutasaidia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kupunguza changamoto ya kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.

Na Mwandishi Wetu

Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe, ameiomba Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati za Foo, Uroki na Romu, ambazo zimeanza kujengwa kwa nguvu na michango ya wananchi.

Saashisha ametoa ombi hilo Agosti 27, 2026, wakati akiuliza swali la nyongeza kwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Riziki Shemdoe, katika Bunge la 13, Kikao cha Pili, jijini Dodoma.

Amesema wananchi wa maeneo hayo wamejitolea kwa kuchangisha fedha, kununua maeneo na kuanza ujenzi wa zahanati, hivyo Serikali inapaswa kuwaunga mkono kwa kutoa fedha zitakazowezesha kukamilisha miradi hiyo.

Sauti ya mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe

Akijibu swali hilo, Waziri wa TAMISEMI Riziki Shemdoe, amesema Serikali inatambua juhudi za wananchi wa maeneo hayo katika kuanza ujenzi wa zahanati hizo.

Shemdoe amesema Mbunge Saashisha Mafuwe tayari amewasilisha barua akiomba Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha zahanati hizo, na kwamba endapo ombi hilo litashughulikiwa na kukamilika, fedha zitatolewa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi.

Aidha, Waziri Shemdoe amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri kuanza kukamilisha angalau zahanati moja kati ya zinazojengwa, ili pale fedha za Serikali zitakapopatikana ziendeleze ujenzi na kuwezesha kukamilishwa kwa zahanati nyingine.  Aidha Shemdoe amempongeza Mbunge Saashisha Mafuwe kwa namna anavyofuatilia masuala ya maendeleo, akisema juhudi hizo zina lengo la kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Hai wanapata huduma bora, ikiwemo huduma za afya

Sauti ya waziri wa TAMISEMI Riziki Shemdoe