Boma Hai FM
Boma Hai FM
28 August 2026, 7:55 am

Mkuu wa Wilaya ya Hai Hassan Bomboko amesisitiza umuhimu wa chanjo ya polio ya matone kwa watoto chini ya miaka 10, huku Mganga Mkuu wa Wilaya akieleza kuwa zaidi ya watoto 63,000 wanalengwa kufikiwa katika kampeni hiyo ,Viongozi wazazi na walimu wahamasishwa pamoja ushiriki wa jamii katika kufanikisha zoezi hilo.
Na Anasta Urio
Hai – Kilimanjaro
Wananchi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuwapa ushirikiano wataalamu wa afya katika utekelezaji wa kampeni ya chanjo ya matone ya polio, kwa kuhakikisha watoto wanapatiwa chanjo hiyo kwa wakati.
Wito huo umetolewa na mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya polio iliyofanyika Agosti 27, 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Hai, ambapo amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapatiwa chanjo hiyo ili kuwalinda dhidi ya ugonjwa wa polio.

Bomboko amesema kinga ni bora kuliko tiba, hivyo Serikali imeamua kuwakinga watoto wenye umri chini ya miaka 10 kama sehemu ya jitihada za kulinda afya ya kizazi cha sasa na kijacho, akisisitiza kuwa chanjo hiyo ni salama kwa afya.
Kwa upande wake mganga mkuu wa Wilaya ya Hai Itikija Msuya, amesema kampeni hiyo inalenga kuwafikia zaidi ya watoto elfu 63 wenye umri chini ya miaka 10 ili wapatiwe chanjo ya polio, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuzuia maambukizi na kuhakikisha taifa linakuwa salama dhidi ya ugonjwa huo.
Naye mwenyekiti Halmashauri ya wilaya ya Hai Edimundi Rutaraka, amewahimiza wananchi kujitokeza katika vituo vilivyopangwa kwa ajili ya chanjo hiyo, akisema chanjo ipo ya kutosha huku akiwataka wanaume kujitokeza kuwasindikiza wanawake katika vituo vya kutolea chanjo ili kutoa ushirikiano katika malezi ya familia na kufanikisha zoezi.

Vilevile mwalimu Nyange Ikwabe wa Shule ya Msingi Bomani, aliyewaleta wanafunzi wake kupatiwa chanjo ya polio, amewataka wazazi kuwa na moyo wa kuipokea chanjo hiyo, akisema lengo la Serikali ni kulinda afya za watoto.

Kwa upande wao, wazazi waliojitokeza katika zoezi hilo, akiwemo Nickolaus Marwa, amewahimiza wazazi wote kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kupata chanjo ya polio kwa ajili ya kuwalinda dhidi ya ugonjwa huo.
Baadhi ya watoto waliojitokeza kupatiwa chanjo hiyo, wakiwemo wanafunzi wa Shule ya Msingi Bomani, Getruda Fadhili na Ikram Said, wamesema wamefika hospitalini ili kupata chanjo itakayowakinga dhidi ya ugonjwa wa polio.
