Boma Hai FM
Boma Hai FM
21 August 2026, 2:22 pm

Madiwani halmashauri ya wilaya Hai wamepongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku wakitaja uwekezaji mkubwa wa serikali katika sekta ya nishati na huduma za kijamii kuwa chachu ya kuboresha maisha ya wananchi.
Na Anasta Urio
Hai – Kilimanjaro
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro limeazimia kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma na maisha ya wananchi katika Wilaya ya Hai.
Azimio hilo limetolewa Agosti 20, 2026, katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai ambapo madiwani wamepongeza serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Diwani wa Kata ya Masama Rundugai, Simbano Aziz amesema uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umewezesha Halmashauri hiyo kutekeleza kwa wakati mipango na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Edmund Rutaraka, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, amesema Halmashauri hiyo iliomba zaidi ya shilingi bilioni 52 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, lakini serikali imefanikisha kutoa zaidi ya shilingi bilioni 55.
Rutaraka alihoji madiwani kuhusu azimio hilo, ambapo madiwani kwa pamoja waliunga mkono hoja ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kile walichokieleza kuwa ni mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ndani ya Wilaya ya Hai na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Hai Hassan Bomboko, ambaye alikuwa mgeni mwalikwa katika kikao hicho, amesema uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umeleta mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo nishati.
Amesema Wilaya ya Hai imevuka lengo la kufikisha huduma ya umeme katika kila kijiji, hatua aliyoeleza kuwa ni sehemu ya mafanikio yanayotokana na uwekezaji mkubwa wa serikali katika sekta ya nishati.
