Boma Hai FM

Wakazi kijiji cha Zarau walalamika ankara kubwa za maji, Meneja Losaa Kia atoa ufanunuzi

1 October 2026, 7:44 pm

Pichani ni mita za maji( picha kwa msaada wa mtandao)

Wakazi wa Zarau wameeleza changamoto wanazokutana nazo kuhusu ankara za maji na mgao wa maji, huku meneja wa Bodi ya maji Losaa Kia Mhandisi Jery Joseph, akitoa ufafanuzi kuhusu utaratibu wa kuhakiki usomaji wa mita kabla ya ankara kutolewa.

Na Bahati Chume & Elizabeth Mafie

Meneja wa Bodi ya maji Losaa Kia Mhandisi Jery Joseph, amesema wananchi wanaopokea  ankara  za maji wanazodhani hazilingani na matumizi yao wanapaswa kuhakiki usomaji wa mita zao mara wanapopokea ujumbe mfupi kutoka bodi hiyo, kabla ya ankara za maji kutolewa.

 Akizungumza na Radio Boma Hai Fm kwa njia ya simu Septemba 30,2026 Mhandisi Jery amesema utaratibu huo umewekwa ili kumwezesha mteja kubaini mapema changamoto kwenye mita au uwezekano wa uvujaji wa maji na kuwasiliana na Bodi kwa ajili ya msaada na kwamba  hatua hiyo imesaidia kupunguza malalamiko katika maeneo mbalimbali kutokana na ushirikiano wa wananchi.

Sauti ya meneja bodi ya maji Losaa Kia mhandisi Jery Joseph akitoa ufanunuzi kufuatia malalamiko ya wakazi wa kijiji cha Zarau.

Ufafanuzi huo umetolewa kufuatia malalamiko ya baadhi ya wakazi wa Kitongoji cha Zarau wilaya  ya Hai, waliodai kupokea ankara kubwa za maji ambazo haziendani na matumizi yao, licha ya kukabiliwa na mgao wa maji.

Akizungumza katika mkutano wa kitongoji hicho uliofanyika Septemba 29 2026, mkazi wa kitongoji hicho John Munisi amesema maji hupatikana kwao mara mbili hadi tatu kwa wiki, hali inayowalazimu kutafuta maji katika maeneo mengine, huku akieleza kuwa hawapati taarifa za kutosha kuhusu sababu ya mgao huo.

Pichani ni wananchi wa kitongoji cha Zarau wakiwa katika kikao cha kitongoji hicho( picha na Bahati Chume)

Kwa upande wake, Mariamu Ibrahimu amesema awali alikuwa akilipa takribani shilingi 4,000 kwa mwezi, lakini tangu mwaka huu anapokea ankara  za hadi shilingi 10,000, jambo analodai halilingani na kiasi cha maji anachotumia.

Nae mwenyekiti wa Kitongoji cha Zarau Michael Mshana, amewataka mafundi wanaosoma mita kuwashirikisha wananchi na kutoa elimu kuhusu usomaji wa mita ili kupunguza malalamiko na kutokuwepo kwa uelewa kuhusu bili.

Pichani ni mwenyekiti wa Kitongoji cha Zarau Michael Mshana katika kikao cha kitongoji hicho.(picha na Bahati Chume)

Akizungumzia mgao wa maji fundi wa maji kutoka Bodi ya Losaa Kia, Nuni Hamidu amesema unatokana na kupungua kwa maji katika vyanzo wakati idadi ya wateja ikiendelea kuwa kubwa.