Boma Hai FM
Boma Hai FM
23 October 2026, 10:41 am

Afisa Mazingira wa wilaya ya Hai Alfred Njegite, amewataka wafanyabiashara kurejea kwenye maeneo rasmi ya biashara na kuzingatia usafi wa mazingira ili kulinda afya za wananchi.
Na Juma Robert
Afisa Mazingira halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Alfred Njegite , amewaomba wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao nje ya maeneo yaliyotengwa kurejea kwenye maeneo rasmi ya biashara ili kurahisisha usimamizi wa usafi na utunzaji wa mazingira.
Akizungumza Oktoba 22 2026, katika kipindi cha Siku Mpya na Radio Boma Hai FM,Njegite ameyataja masoko ya Bomang’ombe na Gezaulole kuwa miongoni mwa maeneo rasmi ambayo wafanyabiashara wanapaswa kuyatumia kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Aidha amewataka wananchi na wafanyabiashara kuchukua hatua na kwenda maeneo yaliyotengwa, pamoja na kusafisha maeneo yao ya kazi na kuepuka kuziba mifereji ya maji ili kuzuia uchafuzi wa mazingira na kupunguza hatari ya magonjwa.
Njegite amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi, akiwataka wananchi kushirikiana na viongozi katika kudumisha usafi wa maeneo ya makazi, biashara na maeneo ya umma ili kuhakikisha Wilaya ya Hai inakuwa safi na salama.