Boma Hai FM

Mikopo ya 10% yachochea uchumi Hai

26 September 2026, 1:43 pm

Pichani ni mratibu  wa mikopo  ya  asilimia 10 katika Halmashauri ya wilaya ya Hai Irene Swale akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa vikundi 49 (Picha na Oliver Joel)

“Jiungeni katika vikundi, wekeni akiba na tumieni mikopo kwa ufanisi.” — Irene Swale

Na Oliver Joel

Hai – Kilimanjaro

Wananchi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kujiunga katika vikundi ili kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Hai bila riba.

Wito huo umetolewa Septemba 25, 2026 na mratibu  wa mikopo  ya  asilimia 10 katika Halmashauri ya wilaya ya Hai Irene Swale, wakati akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa vikundi 49 vilivyokidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo, uliofanyika Kwasadala  kata  ya Masama Kusini, wilayani Hai.

Sauti ya Irene Swale mratibu wa mikopo ya asilimia 10 halmashauri ya Hai

Swale amesema kabla ya mikopo hiyo kutolewa, wanakikundi hupewa elimu kuhusu umuhimu wa kuweka akiba, kutambua aina sahihi za biashara pamoja na kutunza kumbukumbu za shughuli zao za kiuchumi, ili kuwawezesha kutumia mikopo hiyo kwa ufanisi.

Pichani ni Mwezeshaji Samson Hosea ambaye ni Afisa Maendeleo kutoka Kata ya Mnadani akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa vikundi 49 (Picha na Oliver Joel)

Kwa upande wake, Mwezeshaji Samson Hosea ambaye ni Afisa Maendeleo kutoka Kata ya Mnadani, amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuhakikisha wanarejesha fedha kwa wakati ili kutoa fursa kwa wananchi wengine kunufaika na mikopo hiyo.

Sauti ya Mwezeshaji Samson Hosea ambaye ni Afisa Maendeleo kutoka Kata ya Mnadani

Baadhi ya wanufaika akiwemo Justine Emanuel wa kikundi  cha Kihuba na Luvina Tarimo wa Kikundi cha Mtaaluma, wamesema mikopo hiyo imewasaidia kuinua hali zao za kiuchumi baada ya awali kukabiliwa na changamoto za kipato.

Sauti za wanufaika akiwemo Justine Emanuel wa kikundi  cha Kihuba na Luvina Tarimo wa Kikundi cha Mtaaluma
Pichani ni wanavikundi mbalimbali walioshiriki katika mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa vikundi 49 (Picha na Oliver Joel)

Wamesema mikopo hiyo imewawezesha kuanzisha na kuimarisha shughuli zao za kiuchumi, huku wakiwataka wananchi wengine kuchangamkia fursa hiyo ili kujikwamua kiuchumi.