Boma Hai FM

Hai yaweka mkakati kudhibiti maji taka Bomang’ombe

21 August 2026, 1:34 pm

Pichani ni mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka (katikati) Makamu mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Hai Trael Mboya (wa kwanza kulia) pamoja na mkurugenzi mtendaji halmasahuri ya wilaya ya Hai Dionis Myinga( picha na Henry Keto)

Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imeweka mpango wa kuanzisha miundombinu ya majitaka katika Mji Mdogo wa Bomang’ombe, hatua inayolenga kudhibiti utiririshaji holela wa majitaka, kuboresha usafi wa mazingira na kulinda afya za wananchi, huku ukuaji wa mji na shughuli za kiuchumi ukiongeza hitaji la huduma bora za usafi wa mazingira.

Na Vaileth Silvester

Hai – Kilimanjaro

Halmashauri ya wilaya  ya Hai mkoani Kilimanjaro imejipanga kuweka miundombinu ya majitaka katika Mji Mdogo wa Bomang’ombe, hatua inayolenga kuboresha usafi wa mazingira na kulinda afya za wananchi.

Kauli hiyo imetolewa Agosti 20, 2026 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Edimundi Rutaraka, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wakati akijibu swali la Diwani wa Kata ya Bomang’ombe, Evod Njau, kuhusu changamoto ya ukosefu wa mfumo wa majitaka katika eneo hilo.

Rutaraka amesema halmashauri inalipa kipaumbele suala hilo na imeanza kuweka mikakati ya kuhakikisha Mji Mdogo wa Bomang’ombe unapata mfumo bora wa ukusanyaji na uondoshaji wa majitaka ili kukidhi mahitaji ya wananchi na ukuaji wa mji.

Sauti ya mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka

Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kudhibiti utiririshaji holela wa majitaka, kulinda mazingira pamoja na kupunguza hatari ya magonjwa yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira.

Aidha amesema kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na ukuaji wa makazi katika Mji Mdogo wa Bomang’ombe kunahitaji huduma bora za usafi wa mazingira, hivyo halmashauri itaendelea kufuata taratibu na mipango yake katika kutekeleza mradi huo.

Pichani ni madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Hai (picha na Henry Keto)

Miundombinu ya majitaka imeelezwa kuwa ni sehemu muhimu ya maendeleo ya miji, kwani huchangia kuboresha afya ya jamii, kuhifadhi mazingira na kuongeza ubora wa maisha ya wananchi.