Boma Hai FM
Boma Hai FM
22 September 2026, 8:56 am

“Zoezi la usafi liendelee kila siku mpaka mazingira yetu yawe safi, si suala la kufanya usafi leo tu bali ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha eneo lake linakuwa safi.” – Hassan bomboko, Mkuu wa Wilaya ya Hai
Na Richard Salema, Hai kilimanjaro
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko, amewataka wananchi kuendelea na zoezi la usafi wa mazingira na kuondoa miundombinu pamoja na ujenzi uliofanyika kwenye vyanzo vya maji, mitaro na maeneo ya barabara, ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mvua za el nino.
Bomboko ametoa kauli hiyo wakati wa zoezi la usafi, akisema wananchi waliofanya ujenzi katika maeneo ya mitaro, mifereji na pembezoni mwa barabara wataondolewa na kuelekezwa kwenye maeneo rasmi yaliyotengwa na serikali.
Afisa Mazingira wa Wilaya ya Hai, Alfred Njegite, amewapongeza wananchi kwa kushiriki katika zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Njegite amesema zoezi hilo limehusisha kusafisha mitaro, mifereji na maeneo yaliyokuwa na taka, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi katika kudumisha usafi wa mazingira. Amesema usafi unapaswa kuendelea kuwa sehemu ya maisha ya kila siku, badala ya kusubiri siku maalum za usafi.
Mkazi wa Bomang’ombe, Kata ya Bondeni, Yusufu Abraham, amewataka wananchi kuendelea kufanya usafi wa mazingira, hususan kusafisha mitaro na njia za maji, ili kupunguza athari za mvua kubwa zinazotarajiwa.

Abraham amesema usafi ni jukumu la kila mmoja, akiwataka wananchi kufanya usafi kwa hiari na kuchukua tahadhari katika maeneo hatarishi ili kujikinga na maafa pamoja na magonjwa.