Boma Hai FM
Boma Hai FM
22 July 2026, 10:16 am

Watoa huduma za usafiri wa umma wametakiwa kuzingatia haki za abiria kwa kuwapatia tiketi, kuwashusha katika vituo walivyolipia na kufuata taratibu za usalama ili kupunguza malalamiko na kuimarisha huduma kwa wasafiri.
Na Oliver Joel
Hai, Kilimanjaro
Ili kuepuka malalamiko mbalimbali yanayotokana na utoaji wa huduma za usafiri wa umma, watoa huduma wamehimizwa kuzingatia haki za abiria kwa kuwapatia tiketi na kuwashusha katika vituo walivyokusudia.
Wito huo umetolewa Julai 17, 2026 na Sajenti Ramadhani Juma wa Kitengo cha Usalama Barabarani katika Kituo cha Polisi Bomang’ombe alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha Siku Mpya kinachorushwa na Redio Boma Hai FM.
Amesema baadhi ya makondakta wamekuwa na tabia ya kutowashusha abiria katika vituo walivyolipia, jambo linalosababisha usumbufu na malalamiko, huku akisisitiza kuwa kila abiria ana haki ya kushushwa katika kituo alichokusudia kwa mujibu wa sheria.
Aidha Sajenti Ramadhani amewataka wananchi wanaosafirisha mizigo yenye thamani kubwa kutoa taarifa sahihi kuhusu thamani ya mizigo hiyo badala ya kudanganya.
Ameeleza kuwa kutoa taarifa zisizo sahihi kunaweza kumsababishia mhusika kukosa fidia stahiki endapo mzigo utapotea au chombo cha usafiri kitapata ajali au hitilafu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya abiria akiwemo Jacob Charles na Esta kimaro wamesema kuwa wapo baadhi ya makondakta wanaoshusha abiria njiani huku wakieleza kuwa abiria wanapaswa kuwa wakali na kutokubali kushushwa katika vituo ambavyo si sahihi.
Naye Godwin Kiwelu ambaye ni dereva amesema kuwa kwa upande wake hajawahi kushusha abiria kabla ya kumfikisha katika kituo anachoshukia huku akieleza kuwa wapo baadhi ua abiria ambao ndio wanaopenda kushushwa katika vituo visivyo rasmi hali inayoweza kusababisha hatari kama vile ajali.
Ramadhan ambaye ni kondakta ameongeza kuwa endapo ikitokea dharura wanalazimika kuwatafutia usafiri ili waweze kufika vituo wanavyoshukia huku akisema kuwa wakati mwingine,abiria anaweza kulalamika hajashushwa kituo fulani kumbe kituo anachotaka kushuka kikawa hakina kituo rasmi hali inayoweza kuhatarisha usalama wa abiria hivyo huwalazimu kuchukua tahadhari kwa usalama wao na abiria wengine.