Boma Hai FM

Myinga ataka vikundi kutumia mikopo kwa tija na kurejesha kwa wakati

14 June 2026, 8:54 am

Pichani ni wajisirimali mbalimbali walohudhuria katika mafunzo ya mikopo ya asilimia 10 yaliyofanyika shule ya msingi Kibaoni(picha na Juma Robert)

Vikundi mbalimbali vya Wilaya ya Hai vilivyoshiriki mafunzo ya ujasiriamali vimeeleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kusimamia vyema fedha za mikopo, kuandaa miradi yenye tija na kuongeza uwajibikaji katika marejesho ,Mafunzo hayo yamelenga kuhakikisha wanufaika wanatumia mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuongeza kipato cha wanachama na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii na Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa nidhamu ya fedha na urejeshaji wa mikopo kwa wakati ili kuwapa nafasi wananchi wengine kunufaika na mfuko huo.

Na Juma Robert
Hai- Kilimanjaro

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Hai Dionis Myinga ameeleza kuwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri inalenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia shughuli za uzalishaji mali.

Myinga ameyasema hayo Juni 12, 2026 wakati akifunga mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi vinavyo tarajiwa kupewa mikopo ya asilimia 10 yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Kibaoni ambayo yamehusisha vikundi mbalimbali vinavyostahili kunufaika na mpango huo.

Sauti ya Mkurugenzi mtendaji halmashauri wilaya ya Hai Dionis Myinga

Amevitaka vikundi hivyo kufanya kazi kwa malengo ili kuweza kuinuka kiuchumi huku akiwataka kuzingatia taratibu na masharti ya mikopo hiyo, pamoja na kuhakikisha marejesho yanafanyika kwa wakati ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine kunufaika na mfuko huo.

Pichani ni mkurugenzi mtendaji halmasahuri ya wilaya ya Hai Dionis Myinga akizungumza na wajasiriamali mbambali waliojitokeza katika mafunzo hayo(picha na Juma Robert)

Kwa upande wake Tadeo Peter mmoja wa wanufaika walioshiriki mafunzo hayo ameishuru serikali kwa hatua hiyo muhimu inayolenga kuviinua vikundi na kwamba mafunzo hayo yameongeza uelewa kuhusu usimamizi wa fedha, uandaaji wa miradi yenye tija na umuhimu wa kurejesha mikopo kwa wakati ili kuwezesha wananchi wengine kunufaika.

Sauti ya mnufaika Tadeo Piter

Ameongeza kuwa elimu hiyo itasaidia vikundi vingi kutumia fedha za mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa na hivyo kuongeza kipato cha wanachama pamoja na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Pichani ni mnufaika Tadeo Piter(picha na Juma Robert)