Boma Hai FM

Saashisha aomba kujengwa kituo cha afya Muungano

26 June 2026, 6:33 am

Pichani ni mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe(picha kwa msaada wa mtandao)

Katika kuendelea kuhakikisha wananchi wa jimbo la Hai wanapata huduma bora za afya, Mbunge wa jimbo la Hai ameiomba serikali kujenga kituo cha afya kata ya Muungano.

Na Mwandishi wetu

Dodoma

Serikali imeonyesha utayari wa kushirikiana na viongozi wa Jimbo la Hai katika kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuboreshwa, ikiwemo kutenga bajeti na kuanza ujenzi wa vituo vya afya kulingana na vipaumbele na mahitaji ya wananchi.

Hatua hiyo imeelezwa bungeni  Juni 24 ,2026 na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar Sei, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe.

Sauti ya naibu waziri wa ofisi ya waziri mkuu, tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar Sei.

Katika swali lake, Saashisha alitaka kufahamu mpango wa Serikali wa kujenga Kituo cha Afya katika Kata ya Muungano ili kuhudumia wakazi wa kata hiyo pamoja na kata jirani za Bondeni na Bomang’ombe ambazo kwa sasa hazina vituo vya afya.

Sauti ya mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe.

Akijibu hoja hiyo, Dkt. Sei amesema Serikali inapanga ujenzi wa vituo vya afya kwa kuzingatia umbali wa wananchi na idadi ya wakazi katika maeneo husika.

Ameeleza kuwa kwa sasa wananchi wa kata zilizo karibu na Hospitali ya Wilaya ya Hai wanaendelea kupata huduma katika hospitali hiyo, huku akibainisha kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na Mbunge huyo kuhakikisha maeneo yanayostahili yanatengewa bajeti kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vituo vya afya.

Kauli hiyo imefafanuliwa kama ishara ya dhamira ya Serikali kuendelea kuboresha huduma za afya katika Jimbo la Hai, huku wananchi wa Kata ya Muungano na maeneo jirani wakiendelea kupata huduma kupitia Hospitali ya Wilaya ya Hai wakati taratibu za utekelezaji wa miradi ya afya zikizingatia vipaumbele vilivyowekwa.