Boma Hai FM
Boma Hai FM
21 May 2026, 3:01 pm

Mashirika yasiyo ya kiserikali wilayani Hai yamehimizwa kuzingatia sheria, utamaduni wa Kitanzania na uwajibikaji wa kifedha wanapopokea ufadhili kutoka nje, ili kuhakikisha shughuli zao zinaendelea kuleta maendeleo chanya kwa jamii.
Na Juma Robert
Hai-Kilimanjaro
Mashirika yasiyo ya kiserikali wilayani Hai mkoani Kilimanjaro yametakiwa kuhakikisha yanalipa ada kwa wakati pamoja na kulinda mila na desturi za Kitanzania wakati wanapopokea miswada kutoka katika mashirika ya nje yanayotoa ufadhili katika mashirika yao.
Wito huo umetolewa Mei 16, 2026 na mkuu wa divisheni ya maendeleo ya jamii Wilaya ya Hai Robert Mwanga alipokuwa mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko katika mkutano wa mwaka 2026 wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya wilaya ya Hai.
Amesema kuwa yapo baadhi ya mashirika kutoka nje ya nchi yanayotoa ufadhili kwa kuweka masharti yanayokiuka mila na desturi za kitanzania kama vile ushoga,hivyo ameyataka mashirika hayo kuepuka ufadhili huo kwani unaleta athari katika jamii.
Naye Elia Kapinga Mratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali wilaya ya Hai ameyataka Mashirika yasiyo ya kiserikali kufuata kanuni na taratibu za kisheria ili kuweza kuleta maendeleo Chanya kwenye jamii.
Hata hivyo mwakilishi wa Nacongo taifa kutoka mkoa wa Kilimanjaro, Adam Mwashambo amepongeza mashirika hayo na viongozi wake kwa kufanya kazi nzuri ili kuhakikisha mashirika hayo yanaendelea kusonga mbele na kuwahasa kuwa wakurugenzi wa mashirika hayo kuendelea kudhuria mikutano kama huu.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Nacongo wilaya ya Hai Happynesss Eliufoo Kimaro ameyaomba mashirika yasiyo ya kiserikali kuwa na mpango mkakati wa kutembeleana na kufahamiana na kujengeana uwezo wa kupata maarifa tofautitofauti ili kuweza kuinuka katika masuala ya kupata fundi ili kuweza kujiendesha na kusaidia jamii.