Boma Hai FM
Boma Hai FM
9 July 2026, 6:40 pm

Halmashauri ya wilaya ya Hai yapata hati safi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu apongeza, asisitiza utendaji kazi mzuri, upendo na mshikamano na kuwahudumia wananchi kwa upendo na usawa.
Na Riziki lesuya & Henry Keto, Hai-Kilimanjaro
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa kupata hati safi kwa mwaka wa fedha 2024/2025, akisema mafanikio hayo ni uthibitisho wa usimamizi mzuri wa fedha za serikali na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Babu amesema hayo Julai 6, 2026 katika kikao cha Baraza Maalum cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
Aidha, ameielekeza halmashauri hiyo kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Amesema changamoto ya shule chakavu bado inahitaji kipaumbele katika mipango na bajeti za maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka, amemshukuru Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji, madiwani na watumishi wa halmashauri kwa mchango wao ulioiwezesha halmashauri kupata hati safi katika kipindi cha uongozi wake.
Rutaraka amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri wa viongozi na watumishi, huku akisisitiza kuwa halmashauri itaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na matumizi ya fedha ili kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Awali, akisoma taarifa ya ukaguzi, Mkaguzi Mkuu wa Nje wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wenseslaus Nyalusi, amesema ukaguzi huo uliibua mapendekezo 27, ambapo 18 ni mapya na 9 ni ya nyuma. Ameongeza kuwa kati ya mapendekezo hayo, 8 sawa na asilimia 30 tayari yamefanyiwa kazi.