Boma Hai FM

KCEO yapanda miti 1000 shule 6 wilayani Hai

18 April 2026, 2:52 pm

Pichani ni Diwani wa kata ya Machame Kaskazini na makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai Traeli Mboya(kushoto)pamoja na katibu wa KCEO Odette Ngulu wakiwa katika zoezi la upandaji miti shule ya sekondari Hai Day(picha na Elizabeth Mafie)

Katika kuendelea kutunza na kuhifadhi mazingira,shirika la KCEO limefanya zoezi la upandaji miti katika shule sita za wilaya ya Hai.

Na Elizabeth Mafie

Hai Kilimanjaro

Wanafunzi katika shule sita za wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kutunza miti iliyopandwa katika shule zao ili kufikia lengo la utunzaji wa mazingira.

Pichani ni katibu wa KCEO Odette Ngulu akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi(hayupo pichani) picha na Elizabeth Mafie

Wito huo umetolewa Aprili 17, 2026 katika Shule ya Sekondari Hai Day na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Trael Mboya alipomwakilisha Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Edmund Rutaraka katika zoezi la upandaji miti lililofanyika katika shule mbalimbali za wilaya ya Hai ikiwemo Shule ya Hai Day, Bomang’ombe,Mukwasa, Nronga , shule ya wasichana Masama  pamoja na shule ya msingi Mtakuja.

Zoezi hilo limefanywa kwa ushirikiano na Shirika lisilo la kiserikali la Kilimanjaro Community Empowerment Organization (KCEO) lenye makao yake wilayani  Hai  ambalo limefanikiwa kuotesha miti  elfu moja katika shule hizo sita kwa lengo la kuhamasisha utunzaji na ulinzi wa mazingira.

Pichani ni makamu mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Hai Trael Mboya akipanda mti katika shule ya sekondari Hai day( picha na Elizabeth Mafie)

Akizungumza katika zoezi hilo Mboya amesema kuwa ili kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kulinda na kuhifadhi mazingira, ni muhimu kwa wanafunzi kuhakikisha miti hiyo inatunzwa na kukua ili iweze kuleta manufaa ikiwemo kuboresha hali ya hewa na kuongeza uoto wa asili huku akilishukuru shirIka la KCEO kwa kuamua kutunza mazingira kwa kupanda miti katika shule mbalimbali za wilaya ya Hai .

Sauti ya Makamu mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Hai Trael Mboya

Kwa upande wake Katibu wa shirika hilo  Odette Ngulu   amesema lengo la KCEO ni kutunza mazingira  kwa njia mbalimbali mojawapo ikiwa ni kupanda miti  pamoja na kueneza teknolojia rahisi  zinazosaidia kupunguza uharibifu wa mazingira kama kukata miti kwa ajili ya biashara ya mkaa,ili jamii iweze kutumia nishati mbadala  ,kuwa na teknolojia inayowasaidia jamii kufanya biashara na kutengeneza kipato  na kupata uhakika wa chakula na lishe kwa njia rahisi bila kuharibu mazingira.

Sauti ya katibu wa KCEO Odette Ngulu

Ngulu  ameongeza kuwa jamii ya sasa imekuwa ikikata miti kwa ajili ya kupata mkaa na kuni  kwa ajili ya kufanya biashara ili kuweza kuendesha maisha lakini zipo njia mbali mbali za kuweza kujitengenezea kipato ili kuweza kuhifadhi mazingira.

Pichani ni Makamu mwenyekiti Halmashauri ya wilaya ya Hai Trael Mboya (kushoto) pamoja na mkuu wa shule ya Sekondari Hai day mwalimu Alex Warioba.(picha na Elizabeth Mafie)

Naye afisa maliasili  wilaya  ya Hai Mbayani Mollel amesema kuwa wilaya ya Hai miti inapandwa ya kutosha na miti hiyo inastawi na kwamba ofisi ya maliasili wilaya ya Hai imeendelea kutoa elimu katika makundi mbalimbali ili kufanikisha utunzaji wa miti hiyo na mpaka sasa lengo la kupanda miti milioni moja na nusu limetimia kutokana na ushirikiano kuanzia ngazi ya kitongoji ya eneo husika.

Sauti ya afisa maliasili wilaya ya Hai Mbayani Mollel

 Mollel ameongeza kuwa ushiriki wa wanafunzi katika shughuli za mazingira ni hatua muhimu ya kujenga jamii inayojali na kuthamini rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Pichani ni afisa maliasili wilaya ya Hai Mbayani Mollel(wa kwanza kushoto) makamu mwenyekiti halmashauri wilaya ya Hai Trael Mboya(wa pili kushoto) katibu wa KCEO Odette Ngulu(aliyevaa mabuti) mkuu wa shule ya sekondari Hai Day mwalimu Alex Warioba pamoja na wanafunzi mbalimbali walioshiriki katika zoezi la upandaji miti(picha na Elizabeth Mafie)

Miongoni mwa shule zilipanda miti ikiwemo shule ya sekondari Mukwasa na shule ya Sekondari Hai Day wakuu wa shule hizo walipata fursa ya kushukuru shirika la KCEO kwa kuchagua shule hizo na kupanda miti kwani wanafunzi watajisomea katika mazingira tulivu na salama.

Pichani ni Mkuu wa shule ya sekondari Mukwasa mwalimu Castory Kileo akichimba shimo kwa ajili ya kupanda mti katika shule hiyo( picha na Elizabeth Mafie)

Wanafunzi katika shule hizo wamehaidi kutunza miti hiyo na kuifatilia kwa ukaribu ili iweze kuwanufaisha wao na hata wananfunzi wengine watakaokuja kusoma katika shule hizo.

Sauti za wanafunzi kutoka shule mbalimbali zizopandwa miti wilaya ya Hai