Boma Hai FM

Zaidi ya vijana 200 Hai wajengewa uwezo kujitegemea kupitia ujasiriamali

24 July 2026, 12:28 pm

Pichani ni mwenyekiti Halmashauri ya wilaya ya Hai na diwani wa kata ya Muungano Edmund Rutaraka (katikati)na wa kwanza kushoto ni mkurugenzi wa chuo cha elimu kwa wote Savarai Izina pamoja na mtendaji wa kata ya Muungano Andrea Msuya(picha na Bahati Chume)

Washiriki wamehimizwa kutumia ujuzi watakaoupata kuanzisha shughuli za kujiongezea kipato, huku waandaaji wakieleza kuwa ujasiriamali ni njia muhimu ya kupunguza utegemezi wa ajira rasmi.

Na Bahati Chume

Hai – Kilimanjaro

Zaidi ya vijana 200 wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wameanza kunufaika na mafunzo ya ujasiriamali yanayolenga kuwawezesha kujiajiri, kujitegemea na kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira.

Mafunzo hayo yameanza Julai 23 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 25, 2026, katika Chuo cha Kilimanjaro Modern Teachers na Yanaendeshwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Chuo cha Elimu kwa Wote kutoka Dar es Salaam, yakiratibiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Saravai Izina amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kiuchumi na kijamii kwa kuwapa ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kuanzisha shughuli za kujipatia kipato.

Pichani ni mkurugenzi wa chuo cha elimu kwa wote Savarai Izina(picha na Bahati Chume)

“Tunatoa mafunzo ya ujasiriamali ikiwemo utengenezaji wa sabuni, mishumaa na batiki. Tunaamini ujuzi huu utawasaidia vijana kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo badala ya kutegemea ajira pekee,” amesema Izina.

Sauti ya mkurugenzi wa chuo cha elimu kwa wote Savarai Izina.

Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kutumia maarifa watakayopata kuanzisha miradi midogo ya ujasiriamali itakayowasaidia kuboresha maisha yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka, amesema nafasi za ajira serikalini ni chache, hivyo mafunzo ya ujasiriamali ni njia muhimu ya kuwawezesha vijana kujitengenezea ajira na kipato.

Amesema vijana wengi hukosa fursa za kujiajiri kutokana na ukosefu wa maarifa na ujuzi, hivyo mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuwasaidia kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Sauti ya mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Hai na diwani wa kata ya Muungano Edmund Rutaraka.

Naye mkazi wa kata ya Muungano na  mnufaika wa mafunzo hayo Halima Salimu, amempongeza Rutaraka kwa kuratibu mafunzo hayo na kuwezesha vijana kupata elimu ya ujasiriamali itakayowasaidia kujitegemea.

Halima amesema pia Rutaraka ametoa shilingi laki saba ili kugharamia upatikanaji wa vyeti kwa washiriki watakaohitimu mafunzo hayo, hatua ambayo amesema inaonyesha dhamira yake ya kuwawezesha vijana.

Sauti ya mkazi wa kata ya Muungano na mnufaika wa mafunzo ya ujasiriamali Halima Salim

Aidha amewataka washiriki kutumia ujuzi walioupata kwa vitendo kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo zitakazowapunguzia utegemezi kwa wazazi na kuongeza kipato.

Pichani ni Halima Salim mkazi wa kata ya Muungano na mnufaika wa mafunzo.(picha na Bahati Chume)

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameshukuru taasisi hiyo kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali, wakisema itawasaidia kupanga maisha yao na kujiajiri badala ya kusubiri ajira za serikali.

Wamesema mafunzo ya aina hiyo yanapaswa kutolewa kwa vijana wengi zaidi ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea baada ya kuhitimu masomo.

Pichani ni washiriki mbalimbali waliojotokeza kwa ajili ya kupata mafunzo ya ujasiriamali.(picha na Bahati Chume)