Boma Hai FM
Boma Hai FM
3 September 2026, 1:57 pm

Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro imepongeza namna Halmashauri ya Wilaya ya Hai inavyosimamia ukusanyaji wa mapato na miradi ya maendeleo, huku ikieleza kuwa matumizi ya mfumo wa mawakala yanaweza kusaidia kuongeza mapato na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Na Gervas Mosha
Hai – Kilimanjaro
Madiwani na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wameitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa lengo la kujifunza uzoefu wa halmashauri hiyo katika matumizi ya mfumo wa mawakala katika ukusanyaji wa mapato.
Ziara hiyo imefanyika Septemba 2, 2026, ambapo viongozi hao walipokelewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Dionis Myinga kabla ya kufanya kikao katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Hai.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhasibu wa Mapato wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Christopher Manzi, ameeleza namna mfumo wa mawakala unavyotumika katika ukusanyaji wa mapato, pamoja na sababu zilizoifanya halmashauri hiyo kuamua kutumia mfumo huo.
Baada ya kikao, madiwani na wataalamu hao walipata fursa ya kutembelea baadhi ya miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Hai, ambapo walijifunza namna mfumo wa ukusanyaji wa mapato unavyotekelezwa kwa vitendo.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Vicent Lusinde ametoa shukrani na pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa namna inavyosimamia ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kwamba wamejifunza .
Akieleza katika ziara hiyo Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa Beatrice Mwinuka amesema kutokana na mafunzo waliyopata kutoka halmashauri ya wilaya ya Hai kuhusu mfumo wa mawakala katika ukusanyaji wa mapato utaisaidia halmashauri yake kuongeza kiwango cha mapato na hivyo kuiwezesha kutoa huduma stahiki kwa jamii ya wilaya ya kilosa

Naye Diwani wa Kata ya Dumila wilayani Kilosa, Douglas Mwigumila, ameisifu Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa weledi katika usimamizi wa miradi ya maendeleo pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Ziara hiyo inalenga kuwajengea uwezo viongozi na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa kujifunza uzoefu wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai katika kuboresha ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa mawakala.