Boma Hai FM
Boma Hai FM
26 August 2026, 2:58 pm

Viongozi na watu mashuhuri wilayani Hai wametakiwa kuhamasisha wananchi kujenga na kutumia vyoo bora, sambamba na kuhakikisha watoto walio chini ya miaka 10 wanapatiwa chanjo ya polio ili kuzuia maambukizi na kuenea kwa ugonjwa huo.
Na Anasta Urio
Hai – Kilimanjaro
Viongozi mbalimbali na watu mashuhuri katika jamii wametakiwa kuhamasisha wananchi kujenga na kutumia vyoo bora ili kuzuia maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa polio, vinavyoweza kuenea kupitia kinyesi cha binadamu.
Wito huo umetolewa Agosti 24,2026 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai na Afisa Afya wa Kata ya Masama Uroki, Nicholaus Sandale, wakati wa kikao cha kuwajengea uwezo watu mashuhuri kuhusu umuhimu wa chanjo ya polio inayotolewa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 10.

Sandale amesema chanjo ya matone ya polio ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuwalinda watoto dhidi ya ugonjwa huo, akieleza kuwa watoto walio chini ya umri wa miaka 10 ni miongoni mwa kundi lililo katika hatari ya kuambukizwa.
Kwa upande wake, Afisa Afya wilaya ya Hai Fabian Muhibo amesema serikali imeamua kuendelea na utoaji wa chanjo hiyo baada ya kubainika kuwepo kwa maambukizi ya virusi vya polio katika baadhi ya nchi jirani, ikiwemo Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kwamba chanjo hiyo ni hatua muhimu ya kuimarisha kinga kwa watoto na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika jamii.

Naye mjumbe wa baraza la wazee wilaya ya Hai Fransisca Sarimbo amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya vyoo, akisema baadhi ya kaya katika vijiji bado hazitumii vyoo, hali inayoweza kuongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayoambukizwa kupitia kinyesi.
Kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio inafanyika katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwemo Arusha, Dodoma, Mara, Kilimanjaro na Manyara.
Wilayani Hai utoaji wa chanjo hiyo utafanyika kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2026, ikiwa na kaulimbiu “Mpe Chanjo , Zuia Polio.”